Breaking News

ZITTO: NISINGE KAMATWA NINGESHANGAA

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema asingekamatwa na polisi angeshangaa.
Amesema hilo linatokana na kauli ambazo zilitolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali kuhusu takwimu alizotoa.
"Kila mtu alijua tutakamatwa na kama tusingekamatwa basi tungeshangaa,” amesema Zitto leo Jumanne Oktoba 31,2017 baada ya kuachiwa kwa dhamana na polisi.
Zitto amesema maelezo ya kina na ufafanuzi wa kauli zake zinazodaiwa kuwa za uchochezi atayatoa atakapofikishwa mahakamani.
Ufafanuzi mwingine anaodai atautoa atakapofikishwa mahakamani ni kuhusu masuala ya takwimu na makosa ya mtandao.
Pia, amewataka wanachama wa ACT Wazalendo kuendelea na shughuli zao kama kawaida na hasa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017.
Zitto baada ya kuachiwa, mwanasheria wake Stephen Mwakibolwa amesema akiwa Kituo cha Polisi Chang'ombe, mteja wake  alihojiwa kwa kosa la uchochezi alilolifanya wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani Kijichi jijini Dar es Salaam, Jumapili Oktoba 29,2017.
"Pale Chang'ombe alihojiwa kwa uchochezi na baada ya mahojiano aliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kurudi Jumatatu ijayo, lakini baada ya kuachiwa alikamatwa tena na kuletwa hapa (kituo cha polisi cha upelelezi wa makosa ya kifedha)" amesema Mwakibolwa.
Amesema makosa aliyohojiwa akiwa katika kitengo hicho ni kuchapisha au kutoa taarifa zisizo sahihi kinyume cha sheria ya takwimu na kusambaza taarifa za uongo kinyume cha makosa ya mitandao.
Mwakibolwa amesema Zitto amepewa dhamana na kutakiwa kurudi Jumanne Novemba 7,2017.



No comments