Miili ya Watu Waliokufa kwa Kunywa Gongo Yakabidhiwa kwa Mkemia Mkuu
WAKATI idadi rasmi ya watu waliofariki kwa kudaiwa kunywa pombe haramu ya gongo jijini Dar es Salaam ikiongezeka na kufikia 10, Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa miili ya wafu hao imekabidhiwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi.
Hatua hiyo imefikiwa ili kubaini aina ya kemikali (sumu) iliyowasababishia umauti wanywaji wa pombe hiyo ambayo taarifa zisizo rasmi zilidai kuwa ilichanganywa kwa vikorombwezo kadhaa kwa nia ya kuiongezea makali, vikiwamo dawa ya kuondoa madoa maarufu kama Jik na dawa ya kutibu majeraha mabichi aina ya spirit. Uchunguzi huo wa kimaabara wa Mkemia Mkuu unatarajiwa kuanika ukweli wa kila kilichokuwamo kwenye pombe hiyo.
Awali, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliiambia Nipashe juzi kuwa waliofariki kwa kunywa pombe hiyo kwenye eneo la Kimara Stop Over ni watu watano na kueleza kuwa upo uwezekano idadi hiyo kuongezeka kutokana na taarifa walizokuwa nazo kuwa waliokunywa pombe hiyo walikuwa wengi.
Aidha, Mwenyekiti wa Mtaa wa Stop Over, Godfrey Missana, aliiambia Nipashe kuwa wakazi wanane wa mtaa wake walibainika kufariki dunia baada ya pombe hiyo kuwapofua macho, kuwafanya baadhi yao kuendesha na kutapika na mwishowe kufariki dunia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda Mambosasa alisema kuwa hadi kufikia jana mchana, idadi rasmi ya wale waliothibitika kufariki ilifikia kumi na kwamba, miili ya wafu ilikabidhiwa kwa Mkemia Mkuu kwa uchunguzi zaidi wa kitaalamu, pamoja na vielelezo vingine kadhaa kutoka katika eneo la tukio.
Akieleza zaidi mbele ya waandishi wa habari, Kamanda Mambosasa aliongeza kuwa wakati Ofisi ya Mkemia ikiendelea kutafuta chanzo cha vifo hivyo, jeshi hilo linaendelea kumsaka mtuhumiwa aliyewauzia watu pombe hiyo haramu.
“Tunaendelea kumsaka mtu aliyewauzia pombe hiyo watu hawa waliopoteza maisha. Katika eneo la tukio ziliokotwa chupa tatu za ujazo wa lita moja zikiwa zimejazwa pombe inayodhaniwa kuwa ni haramu ya gongo,” alisema Mambosasa.
Aidha, akieleza namna ilivyokuwa, Kamanda Mambosasa alisema kuwa juzi alfajiri, walipokea taarifa kutoka kwa Matigo Ramadhani (38), ambaye ni mkazi wa Kimara Stop Over, akiwaeleza kuwa ndugu yake, Maleo Ramadhani (45), alirudi nyumbani akilalamika kuumwa tumbo, kuishiwa nguvu huku akiwa na kizunguzungu na kumweleza kuwa alikunywa pombe ya kienyeji kwa mama Anoza.
Alisema Matigo aliitaarifu polisi kuwa, walimpeleka ndugu yao Hospitali ya Mwananyamala na kupatiwa matibabu kisha walirudi naye nyumbani lakini alifariki dunia usiku wa siku hiyo.
“Baada ya muda alijitokeza mtoa taarifa mwingine aitwaye Paula Kisangila (53), mkazi wa Stop Over pia…naye alieleza kuwa aliporudi nyumbani kwake usiku akitokea kwenye shughuli zake, hakumkuta mlinzi wake aliyemtaja kwa jina moja la Yona anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 hadi 30,” alisema.
Alisema kisangila alidai kuwa baada ya kumtafuta mlinzi huyo, walimkuta akiwa amefariki nje ya uzio wa nyumba.
Kamanda Mambosasa alisema walipata taarifa ya kuwapo kwa miili mingine saba katika Hospitali ya Mwananyamala na ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani ambayo ni ya Mohamed Issa (67), mkazi wa Kimara Saranga; Kabugh Rashidi (64), Stanslaus Joseph (58), Stephen Isaya (61) na Monica Rugaillukamu (42), wote wakiwa ni wakazi wa Kimara Saranga.
Kamanda Mambosasa aliwataja marehemu wengine katika tukio hilo kuwa ni Alex Madega, (41) mkazi wa Kimara Korogwe; Hamisi Mbala (35), mkazi wa Kimara Golani na Ekson Nyoni (28), mkazi wa Kimara Stop Over.
MWENYEKITI, MTOTO WA MAREHEMU
Juzi, mwenyekiti wa Mtaa wa Stop Over, Missana, aliiambia Nipashe kuwa kabla ya watu hao kufariki dunia, kulikuwa na taarifa kuwa baadhi yao walianza kulalamika macho yao kuwa mekundu sana, kuwauma na mwishowe kupoteza uwezo wa kuona ghafla kabla ya kukimbiziwa hospitali na majirani.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, alisema kuwa pombe hiyo huuzwa katika kibanda kimoja kwenye eneo hilo na kwamba, miongoni mwa waliokufa ni pamoja na muonjaji ajulikanaye kwa jina la Mama Ramahuku mmiliki anayefahamika kwa jina la Dada Anoza akikimbilia kusikojulikana akihofia kukamatwa na Polisi.
Paulina Joseph, ambaye ni mtoto wa marehemu Joseph, aliiambia Nipashe juzi kuwa kabla ya kufariki dunia, baba yake alimkuta amezidiwa na kila mara alikuwa akimsindikiza chooni kutokana na kuendesha huku pia akilalamika macho yake kutoona tena.
No comments