Breaking News

KIGWANGALA ATOA SIKU 30 TARIME


Kigwangallah akiwa katika ziara yake wilayani hapo ya kuvitembelea vituo vya afya, zahanati na hospitali ya wilaya hiyo, alisema licha ya kuwa na majengo mazuri, lakini yanakuwa hayana maana kama hakuna mashine hizo kwa kipindi cha miezi tisa sasa.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangallah, ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara kutengeneza mashine mbili za maabara ya hospitali hiyo.

Kigwangallah akiwa katika ziara yake wilayani hapo ya kuvitembelea vituo vya afya, zahanati na hospitali ya wilaya hiyo, alisema licha ya kuwa na majengo mazuri, lakini yanakuwa hayana maana kama hakuna mashine hizo kwa kipindi cha miezi tisa sasa.

Alizitaja mashine hizo zinzochunguza magonjwa yote ya kuambukiza kama Ukimwi, homa ya ini, homa ya manjano, ebola na yale ya mlipuko kama kipindupindu.

“Watumishi kwenye maabara wapo tu wamejazana hawana kazi ya kufanya kwa sababu hakuna vitendea kazi, wakati Serikali inatoa pesa za vitendanishi zinaliwa,” alisema Dk Kigwangallah.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Calvin Mwasha alisema mashine hizo ziliharibika na hakuna fedha ya kuzitengeneza huku akidai kuwa fedha za vitendanishi hutumika katika maeneo mengine yenye upungufu.

Hata hivyo, Dk Kigwangallah alisema hairuhusiwi fedha kuhamishiwa kwenye matumizi mengine.

Mkazi wa Tarime, Roza Marwa alisema licha ya kutoa fedha za mfuko wa hifadhi ya jamii na pesa za papo kwa papo Sh6,000 lakini wanapohitaji vipimo vya maabara hutakiwa kuvilipia.

Mkazi wa Sabasabasaba, Mwita Marwa alisema inasikitissha kuona hospitali kubwa kama hiyo inakosa mashine hizo, hivyo kuwasababishia usumbufu mkubwa wagonjwa wanaohitaji huduma.

Marwa aliwataka watendaji kuhakikisha kuwa kila kitu kinakuwa vizuri hospitalini hapo.

Pia, Dk Kigwangallah aliwataka wakurugenzi wa halmashauri ya wilaya na ile ya mji kuhakikisha vituo vyote vya afya na wilaya vinakuwa na mifumo ya maji kwenye wodi zote muhimu.


No comments