Breaking News

BILIONEA ERASTO MSUYA-Shahidi: Simu ya marehemu ilitusaidia kunasa watuhumiwa

Akitoa ushahidi wake jana, koplo Faraji ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa makosa ya kimtandao, alidai kuwa simu ya Msuya (marehemu) ilikutwa na ujumbe (SMS), uliomvuta kwenda eneo la tukio.

Moshi. Shahidi wa 11 wa upande wa mashtaka, koplo Seleman Faraji ameiambia Mahakama Kuu Kanda ya Moshi namna simu ya marehemu ilivyosaidia kuwakamata washtakiwa katika kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya.

Akitoa ushahidi wake jana, koplo Faraji ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa makosa ya kimtandao, alidai kuwa simu ya Msuya (marehemu) ilikutwa na ujumbe (SMS), uliomvuta kwenda eneo la tukio.

Katika ushahidi wake huo alioutoa kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Lucy Kyusa shahidi huyo alidai kuwa katika kufanikisha mpango huo, zilisajiliwa namba mpya tano za simu kwa siku moja.

Alidai Agosti 7, 2013, alikabidhiwa simu za marehemu aina ya Samsung Galaxy S4, iphone 5 na tablet moja kwa ajili ya uchunguzi na kufanikiwa kuondoa neno la siri kwenye simu ya iphone.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, baada ya kuondoa neno la siri, walibaini simu ya marehemu ilifanya mawasiliano na namba ya simu ya Airtel 0682 405323 ikimuelekeza Msuya kabla ya kifo chake, kwenda eneo la tukio.

Katika uchunguzi huo, walibaini simu hiyo ilisajiliwa kwa jina la Motii Mongulu na wakala aliyeko stendi kuu ya mabasi Jijini Arusha na ilikuwa ikiwasiliana na namba zingine nne.

Sehemu ya mahojiano kati ya Wakili Kyusa anayesaidiana na mawakili waandamizi wa Serikali Abdalah Chavula na Omary Kibwana na Wakili wa Serikali Nassir Kasim na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:-

Wakili Kyusa: Mlipoichunguza namba iliyowasiliana na marehemu mlibaini vitu gani?

Shahidi: Nilibaini imesajiliwa stendi ya mabasi Arusha siku moja kabla ya tukio na ilikuwa ikifanya mawasiliano na namba nyingine nne tu ukiacha ile ya marehemu.

Wakili Kyusa: Vitu gani vingine mligundua?

Shahidi: Tulifuatilia zile namba nyingine nne na kugundua zote zilisajiliwa siku moja kwa majina ya kimasai ya Motii Rilia, Motii Siria na Oldonyo Olpiloli.

Wakili Kyusa: Baada ya kubaini, mlichukua hatua gani?

Shahidi: Tulikwenda Arusha kumfuatilia wakala aliyesajili laini hizo.

Wakili Kyusa: Nini kiliendelea?

Shahidi: Tulifika Arusha na kumpata wakala na bahati nzuri alikuwa mdada anaitwa Hamisa. Alizitambua zile namba na akasema zilisajiliwa na rafiki yao anayemtambua kama Masai au Adam.

Wakili Kyusa: Baada ya kupata taarifa hizo mlifanya nini?

Shahidi: Hamisa alitupatia namba ya simu ya Adam.

Wakili Kyusa: Baada ya kupata namba ya Adam au Masai nini kilifuata?

Shahidi: Tulifuatilia location (mahali) ya hiyo namba na ilisomeka iko Mirerani.

Wakili Kyusa: Nini kilifuata?

Shahidi: Tulifika Mererani tukiwa na timu ya ukamataji na kuweka mitego.

Wakili Kyusa: Mliweka mitego gani hadi kumkamata?

Shahidi: Tulitumia third party (mtu wa tatu).

Wakili Kyusa: Tupeleke sasa kwenye eneo la tukio, mlifanyaje?

Shahidi: Baada ya kumpata third party tukafanikiwa kumpata Adam.

Wakili Kyusa: Baada ya kumpata Adam aliwaambia nini?

Shahidi: Alikubali kusajili zile namba kwa maelekezo ya dereva wao aliyemtaja kuwa ni Mussa Mangu (mshtakiwa wa tatu).

Wakili Kyusa: Nini kilifuata?

Shahidi: Alituambia hata wakati wa kwenda kusajili hizo laini walikwenda naye na akatupatia simu ya Mussa Mangu.

Wakili Kyusa: Nini kilifuata baada ya kupata namba hiyo ya simu?

Shahidi: Tuliwasiliana na Service Provider (mtoa huduma) ili kupata location yake na tulibaini kwa wakati huo alikuwa maeneo ya KIA.

Wakili Kyusa: Nini kiliendelea?

Shahidi: Nilimpigia simu na kuweka mitego ya kukutana naye.

Wakili Kyusa: Uliweka mitego gani?

Shahidi: Nilijifanya ni ofisa wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na akasema anatoka KIA hivyo tukutanie Arusha.

Wakili Kyusa: Baada ya kuweka mitego hiyo nini kilifuata?

Shahidi: Tuliongozana na timu ya ukamataji hadi Arusha na kufanikiwa kumkamata Mussa.

Wakili Kyusa: Baada ya kumkamata nini kilifuata?

Shahidi: Tulimkabidhi kwa timu ya mahojiano.

Wakili Kyusa: Baada ya hapo nini kilifuata?

Shahidi: Tarehe 11.8.2013 Inspekta Samwel (Maimu-shahidi wa tisa) alituletea namba za simu na majina ya washirika wa mauaji waliotajwa katika mahojiano.

Wakili Kyusa: Yalikuwa ni majina gani?

Shahidi: Nakumbuka tuliletewa majina na namba za Sadick, Karim, Jalila, Ally na Shaibu.

(Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne au Mredii, Mussa Mangu, Jalila Zuberi au Said, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed au Msudani na Ally Mussa au Mjeshi).

Wakili Kyusa: Baada ya kupata namba hizo, mlifanyaje?

Shahidi: Tulizichunguza na zilikuwa zinasomeka location tofauti. Jalila na Ally walikuwa Babati; Karim na Sadick walikuwa wanasomeka Dar es Salaam na Shaibu alikuwa yuko Mererani.

(Kwa mujibu wa shahidi huyo, baada ya kupata maeneo walipo watuhumiwa, waliwafuatilia na kufanikiwa kuwakamata ingawa wengine walikuwa wamehama maeneo waliyokuwapo awali).

Shahidi huyo aliiambia Mahakama kuwa Agosti 16,2013 baada ya kumkamata mshtakiwa wa pili, (Shaibu) huko Mirerani, alipewa jukumu la kuandika maelezo yake katika kituo cha polisi Mirerani.

Alidai kuwa katika maelezo hayo ambayo alisema aliyatoa kwa hiyari yake na bila kulazimishwa na mtu yeyote, mshtakiwa huyo alikiri kushiriki katika tukio la kumuua mfanyabiashara huyo.

Hata hivyo, shahidi huyo alipoiomba Mahakama ipokee maelezo hayo kama kielelezo cha kesi hiyo, jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa na Majura Magafu lilipinga na kutoa sababu kuu nne.

Akiwasilisha sababu hizo, wakili Magafu alisema mshtakiwa amemweleza kuwa hakuwahi kuandika maelezo yake polisi Agosti 16, 2013 kwa vile siku hiyo alikuwa bado hajakamatwa na polisi.

Pia, wakili Magafu alisema mshtakiwa anasema anachojua ni kuwa Agosti 18, 2013 ndipo alipoteswa na polisi na kulazimishwa kusaini maelezo ambayo hakuyatambua.

Mbali na sababu hiyo, wakili Magafu alisema maelezo aliyolazimishwa kuyasaini na kuweka dole gumba, hakuwahi kusomewa wala kujua kichokuwapo na wala hajui chochote kuhusiana na tukio hilo.

Katika sababu ya nne, wakili Magafu alidai kuwa baada ya mshtakiwa kuteswa na kuumizwa, polisi waliingiwa na woga angeweza kufia kituo cha polisi Moshi, hivyo Agosti 21 wakampeleka hospitali.

Wakili Magafu alidai kuwa mshtakiwa alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi na baadaye kuendelea kutibiwa katika Zahanati ya Gereza la Karanga hadi alipozidiwa na kupelekwa Hospitali ya KCMC.

Baada ya kutoa hoja hiyo, wakili wa Serikali mwandamizi, Abdalah Chavula alisema msimamo wa kisheria linapojitokeza suala la mshtakiwa kama alitoa maelezo kwa hiyari au la, lazima kuwapo kesi ndani ya kesi.

Akitoa ushahidi wake katika kesi ndani ya kesi, shahidi wa kwanza ambaye ni koplo Faraji alisisitiza kuwa wakati akichukua maelezo yake, mshtakiwa alikuwa na afya njema na hakuwa na jeraha lolote.

Baadaye mawakili wa utetezi walipata nafasi ya kumhoji koplo Faraji na sehemu ya mahojiano kati ya wakili Hudson Ndusyepo na wakili Magafu na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:-

Wakili Ndusyepo: Tarehe 16.8.2013 mshtakiwa uliyekuwa ukimchukua maelezo, ulijua weledi wake?

Shahidi: Alisema ana elimu ya darasa la saba na anajua kusoma na kuandika.

Wakili Ndusyepo: Wakati anayeleza yote kuhusiana na tuhuma hizi, alieleza kwa hiyari yake?

Shahidi: Alieleza kwa hiyari yake mwenyewe.

Wakili Ndusyepo: Kama mtuhumiwa alikuwa anaeleza, kwanini hukumpa karatasi aandike mwenyewe?

Shahidi: Ni uchaguzi wa mimi kama mpelelezi kuamua nitumie kifungu cha 57 niandike maswali na majibu kama nilivyofanya au nitumie kifungu cha 58 na kumpa karatasi na kalamu.

Wakili Magafu: Kuna wakati wowote ule timu ya upelelezi ilimhoji kabla ya wewe kumuandika maelezo.

Shahidi: Sikuwahi kusikia hilo.

Wakili Magafu: Wewe binafsi uliwahi kuandika maelezo yako katika hii kesi?

Shahidi: Ndiyo niliandika.

Wakili Magafu: Hebu tizama hii document (nyaraka) halafu useme kama unaitambua.

Shahidi: Hii ni karatasi ya maelezo yangu.

(Wakili Magafu alitumia maelezo hayo kumbana shahidi huyo kuonyesha kuwa wakati anaandika maelezo ya mshtakiwa, tayari alikuwa amejulishwa kuwa alishahojiwa na timu ya wapelelezi).

Kesi hiyo itaendelea Jumatatu, upande wa mashtaka utaita mashahidi zaidi kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitoa maelezo hayo ya kukiri kosa kwa hiyari pasipo kuteswa na polisi.

No comments