Breaking News

Serikali yatoa kauli uuzaji mapanga, sime Ubungo Mataa


Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema wafanyabiashara wa silaha za jadi barabarani watadhibitiwa.

Serikali imesema uuzaji wa silaha za jadi holela upo katika maeneo mbalimbali hivyo kusababisha zizagae na kutumika vibaya.

Maeneo yaliyotajwa kushamiri kwa uuzaji wa silaha hizo ni barabarani, ikiwemo kwenye makutano ya barabara za Mandela na Morogoro eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusufu Masauni amesema Jeshi la Polisi linatambua uwepo wa tatizo hilo na hatua zimeanza kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Maryam Msabaha aliyetaka kujua Serikali inalichukuliaje suala la uuzaji wa silaha za jadi holela kama vile  mapanga na visu katika maeneo ya Ubungo Mataa hali inayotia hofu wananchi.

Naibu waziri ametaja hatua zilizochukuliwa ni kufanya operesheni ya mara kwa mara ya kuwakamata wauzaji wa silaha za jadi barabarani kama vile mapanga, mikuki, pinde na mishale.

Amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka zingine serikalini limeandaa utaratibu maalumu wa uuzaji wa bidhaa za aina hiyo na kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya biashara hiyo.

Masauni amewashauri wananchi waipige vita na kuepuka kujihusisha na biashara hiyo.

No comments