MWIJAGE AKATA TAMAA TANZANIA YA VIWANDA
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage ameonyesha wasiwasi Tanzania kuwa na viwanda endelevu kama serikali itashindwa kutoa fedha ambazo iliombwa na wizara hiyo ya viwanda katika kutekeleza na kukuza viwanda nchini Tanzania.
Waziri Mwijage amesema hayo leo bungeni wakati akijibu swali lililoulizwa na mbunge Viti Maalum Kiteto, Zawadi Koshuma ambaye aliuliza kama ujenzi wa viwanda unaweza kutimia ikiwa serikali haitekelezi na kutoa fedha zilizoobwa na Wizara husika kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa viwanda hivyo vidogovidogo.
"Napenda nikiri na nakubaliana naye Mhe. Koshuma ujenzi wa uchumi wa viwanda endelevu unatokana na viwanda vinavyoitwa LGI (Local Grown Industry) siyo hizi (FDI) hawa wanatafuta 'greener pastures' wataondoka na serikali inalitambua hilo. Mwaka jana tulitakiwa kupewa 2.5 bilioni hatukupewa, tumeiomba serikali tupewe 7.04 bilioni nina imani serikali itatoa fedha hizo na nitafuatilia, napenda niishie hapo na kamati yangu imefanyia kazi na tusipotoa hizo fedha hivi viwanda tunavyoviita FDI hao ni kwale, huwezi kulisha kwale ukaacha watoto wa kuku naomba niishie hapo" alisisitiza Mwijage.
Kwa mujibu wa mbunge Viti Maalum Kiteto, Zawadi Koshuma (CCM) amesema kuwa serikali imekuwa ikitenga fedha lakini imekuwa haitekelezi kwani mwaka 2015/2016 ilitenga milioni mia tano mwaka 2016/17 ilitenga bilioni 2.4 lakini mwaka 2017/18 serikali imetenga bilioni 7 lakini serikali imekuwa haipeleki fedha hizo jambo ambalo limafanya wawe na hofu kuwa kauli mbiu ya Tanzania na viwanda inaweza isiwepo kama fedha hizo zitakuwa hazipelekwi kwa ajili ya kufanya utekelezaji
No comments