MWIGULU AIBUA UPYA ALIYEMTOLEA BASTOLA NAPE NAUYE
Waziri Mwigulu alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds baada ya mmoja wa wasikilizaji kutaka kujua kama mtu huyo aliyemtolea bastola Nape alikamatwa au hajakamatwa.
Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kwamba mtu aliyemtolea bastola hadharani Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye si askari wa Jeshi la Polisi imeibua upya mjadala kuhusu suala hilo.
Waziri Mwigulu alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds baada ya mmoja wa wasikilizaji kutaka kujua kama mtu huyo aliyemtolea bastola Nape alikamatwa au hajakamatwa.
VIDEO HIYO HAPO
Baada ya kauli hiyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wametaka waziri Mwigulu ambaye Jeshi la Polisi liko chini yake kuueleza umma mtu huyo kama si askari ni nani au awachukulie hatua askari
walioshindwa kumchukulia hatua mtu huyo.
Nape alikumbana na kadhia hiyo Machi 23 ikiwa ni saa chache kupita tangu Rais John Magufuli alipotangaza kumwondoa kwenye Baraza la Mawaziri akihudumu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Baada ya kuondolewa asubuhi, siku hiyohiyo mchana Nape alipanga kufanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam ambako alikuta zuio la vyombo vya dola na alipolazimisha alijikuta akitolewa bastola mbele ya waandishi wa ndani na nje akitakiwa kurudi ndani ya gari lake na asifanye mkutano huo.
Tangu kutokea kwa tukio hilo, kumekuwapo mijadala hasa ikilenga kujua kwa nini hatua hazichukuliwi kwa mtu huyo licha ya video na picha mbalimbali zinazomwonyesha akitoa bastola na kumnyooshea Nape zipo na zinasambaa mitandaoni.
Mjadala huo ulitua katika Bunge la Bajeti lililokutana Aprili na hata katika mkutano wa Bunge uliomalizika wiki tatu zilizopita mjini Dodoma, baadhi ya wabunge wakitaka suala hilo na matukio mengine yajadiliwe ndani ya Bunge jambo ambalo halikufanyika.
Spika wa Bunge, Job Ndugai alichukua uamuzi wa kuitaka Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake, Balozi Adadi Rajabu kulishughulikia suala hilo na taarifa yake ilikuwa isomwe katika mkutano huo wa Bunge lakini ilishindikana na inatarajiwa kusomwa Novemba.
Juzi, waziri Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi akijibu swali la msikilizaji kuhusu mtu huyo kukamatwa au la akisema: “Ninachofahamu aliyemtishia bastola Nape hakuwa polisi kama ambavyo ilidhaniwa.”
Alisema katika tukio kama hilo, wahalifu wanaweza kutumia nafasi hiyo kufanya watakavyo, lakini uchunguzi wa suala hilo unaendelea.
Jana, gazeti hili lilimtafuta Nape kutaka kujua maoni yake kuhusu kauli ya waziri Mwigulu ambaye alisema kwa kifupi: “Siwezi kuzungumzia hilo kwani sijaona… nikiona nitaweza kuzungumza.”
Itakumbukwa, Aprili 8 mwaka huu, Nape akizungumza jimboni kwake kwa mara ya kwanza tangu alipoondolewa katika nafasi ya uwaziri alisema hakuchaguliwa kwenda kuwa waziri bali kuwatumikia wananchi huku akitoa ushauri kwa Rais Magufuli.
“Namwomba Rais wangu, na huu ni ushauri tu, simlazimishi, ninampa ushauri na kumwomba… kwa sababu matendo haya yanamjengea chuki yeye na wananchi kwa sababu wanadhani yeye ndiye anaowatuma,” alisema.
Nape alisema, “Sasa ili Rais wangu asijengewe chuki lazima ajiondoe kwenye jambo hili na namna ya kujiondoa ni kuunda tume iende kuchunguza imletee ripoti nani yupo nyuma ya haya matendo ya kihuni.” Alisema, “Ili atenganishe CCM na matendo ya wahuni wachache wanaotumia dhamana waliyopewa kuumiza watu na kupoteza watu lazima tume iundwe iende ikatuletee ukweli, ngoja niseme hapa kwani si nipo nyumbani tu… kama nilitolewa bastola si ni sawa na kufa tu, basi nipo tayari.”
Atueleze ni nani
Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), John Seka akizungumza na gazeti hili kuhusu kauli ya waziri Mwigulu alisema inaashiria kwamba uchunguzi wa suala hilo la Nape umekamilika hivyo taarifa yake inapaswa kutolewa kwa wananchi.
“Kama waziri amesema si askari, anawajibu wa kusema ni nani, kwani ushahidi wa mazingira upo. Lakini kama hakuwa askari alikuwa ni nani, je, anaruhusiwa kumiliki silaha na je, alitumwa na nani kwa lengo gani,” alihoji Seka.
Alisema, “Na kauli hiyo ya waziri inaashiria uchunguzi umekamilika na kubaini kwamba si askari… nilitarajia jana (juzi) wangemuuliza pale kama si askari wa Jeshi la Polisi ni nani kwani kwa kauli hiyo uchunguzi unaonesha umekamilika.”
Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu alisema: “Siwezi kuyazungumzia masuala hayo katika simu, ‘next week’ nitakuwa bungeni Dodoma utanitafuta.”
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Ernest Mangu alisema, “Sina hiyo fursa, waulize walio kwenye nafasi hiyo.”
Alipoulizwa kwamba anaweza kutoa maoni yake na yakafanyiwa kazi ili huyo asiyejulikana akajulikana, Mangu alisema, “Kama watahitaji wataniuliza, wewe unaniuliza kama nani, hayo ni masuala ya kiutendaji.”
Polisi wawajibishwe
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Onesmo ole Ngurumwa alisema kauli ya waziri Mwigulu inazua utata hasa ikizingatiwa Nape alizuiwa kufanya mkutano na aliyetoa bastola aliitoa mbele ya askari wakishuhudia.
“Kitendo cha yule kutoa silaha mbele ya askari tena na RPC Kaganda (aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda) alikuwepo na akaachwa inaonyesha wanamjua ni mwenzao, kama si mwenzao au hawamjui, ilikuwaje atoe silaha hadharani na wamwache bila kumchukulia hatua,” alihoji.
Ole Ngurumwa alisema, “Kama ndivyo, basi Mwigulu awachukulie hatua askari wake waliokuwepo wakati huyo asiyejulikana anatoa bastola kwani ni kosa kutoa silaha hadharani tena mbele ya askari.”
Kauli ya kwanza ya Mwigulu
Itakumbukwa Machi 24 ikiwa ni siku moja tangu Nape kunyooshewa bastola, waziri Mwigulu alitumia akaunti yake ya mtandao wa kijamii kuzungumzia sakata hilo akisema, “Mh. Nape Moses Nnauye sio jambazi, ni Mtanzania, ni mbunge, mjumbe wa NEC wa CCM, hana record ya uhalifu.”
“Kitendo cha mtu kumtolea bastola, sio cha kiaskari, sio cha Kitanzania na sio cha ki Mungu, kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya kamera nawaza mbali ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini,” alisema.
Alisema, “Nahusika na usalama wa raia wote wa Tanzania, nimemwelekeza IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya uaskari, na kama ni askari basi sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake,” alisem
No comments