Breaking News

Waziri Mkuu Ampa Siku 15 Mweka Hazina Sikonge Ataka apate maelezo kwa nini ameshindwa kukusanya mapato

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa siku 15 Mweka Hazina wa Wilaya ya Sikonge, Bw. Evans Shemdoe ajieleze ni kwa nini ameshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya ndani.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo asubuhi (Alhamisi, Agosti 10, 2017) wakati akizungumza na watumishi na watendaji wa wilaya hiyo, mjini Sikonge.

“Nataka maelezo yakayoniridhisha ni kwa nini hamkufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya halmashauri ambacho ni kiwango cha chini. Nzega TC wamefikisha asilimia 112, Kaliua wana asilimia 91, Nzega DC wana asilimia 80, ni kwa nini wewe umeshindwa kufikisha kiwango hicho?,” alihoji Waziri Mkuu.

“Ninataka nipate maelezo pia ni ipi mipango yenu ya kukusanya mapato kwa maeneo mliyoshindwa kufanya vizuri, na pia mmejipangaje kwa mwaka ujao wa fedha. Niyapate maelezo hayo ifikapo tarehe 25 Agosti,” amesema.

Alipopewa nafasi ya kujieleza, Bw. Shemdoe alisema wamefikisha asilimia 76.7 na wameshindwa kufikia lengo kwa sababu ya upungufu wa mvua katika msimu uliopita, hali ambayo ilichangia kushuka kwa mavuno ya zao la tumbaku miongoni mwa wakulima.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa wilaya hiyo, washirikiane na watendaji na madiwani ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala ya kuwaachia watendaji wa kata peke yao.

Jana, mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Tabora, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri tano kati ya nane za mkoa huo zitoe maelezo ni kwa nini zimeshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo kama ambavyo waliagizwa na Serikali.

“Halmashauri zilizovuka malengo ni tatu tu, Nzega TC, Kaliua na Nzega DC. Nataka taarifa za halmashauri zilizobakia ifikapo Agosti 25, wakijieleza ni kwa nini hawajafikia malengo ya ukusanyaji mapato yaliyowekwa ambayo ni asilimia 80,” alisema.

Taarifa ya mkoa huo inaonyesha makusanyo kwa kila Halmashauri ni kama ifuatavyo:- Tabora Manispaa asilimia 64.1; Nzega Mji (asilimia 112); Nzega Wilaya (asilimia 80.8); Igunga (asilimia 64.6); Tabora (asilimia 77.3); Sikonge (asilimia 76.7); Urambo (asilimia 70.9) na Kaliua (asilimia 91.5).

Pia amezitaka Halmashauri zote zihakikishe zinafanyamakusanyo kwa kutumia mfumo wa kielektroniki. “Ukusanyaji wote wa mapato ni lazima ufanyike kwa mfumo wa kielektroniki. Halmashauri ambazo hazijafanya hivyo, zitumie makusanyo ya mwaka jana kununulia mashine za EFD. Hatutaki kuona risiti za kuandika kwa mkono zinatumika,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa wa Tabora uhakikishe wanapatikana watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika wilaya hiyo ili waweze kusaidiana na watendaji wa halmashauri hiyo kukusanya mapato.

“Hapa Sikonge naambiwa hakuna ofisi za TRA. Lazima tupate maafisa wa TRA katika kila Halmashauri ili watoe elimu na washirikiane na madiwani, watendaji wa vijiji na watumishi wa Halmashauri juu ya ukusanyaji mapato,” alisema.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, AGOSTI 10, 2017.

No comments