Breaking News

Lissu bado anashikiliwa na Polisi

Mbunge  wa Singida Mashariki Tundu Lissu 

Wakili Frederick Kihwelo amesema kwamba anashangaa inakuwaje mpaka sasa hajafikishwa mahakamani

Dar es Salaam.Wakili Frederick Kihwelo amesema mteja wake Tundu Lissu ameendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Kituo cha Kati hadi muda huu( 5:50) na hakuna dalili za kufikishwa mahakamani kama walivyokubaliana jana.

Kihwelo ameliambia gazeti hili kwamba, jana maofisa wa Polisi walimuhakikishia kwamba leo angefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma zinazomkabili.

Jana, mawakili wa mbunge huyo wa Singida Mashariki walishindwa kufanikisha dhamana na alilala rumande huku polisi wakitumia saa moja na nusu kumpekua Lissu nyumbani kwake,wakitafuta nyaraka zinazohusiana na kushikiliwa kwa ndege hiyo.

"Bado tunaendelea kufuatilia lakini ikifika mchana,kuanzia saa 8:00 tutachukua hatua nyingine kama hawatakuwa wamemfikisha mahakamani, leo tumefika mahakamani asubuhi tukijua watamleta huku(Kisutu) kama tulivyokubaliana lakini hakuna dalili,"amesema  Kihwelo.

"Hatujafahamu nini kilichosababisha wasimfikishe hadi sasa.tutawasiliana baadaye kwa hatua zaidi, tunaweza kuiomba mahakama iwaamuru wamfikishe mahakamani." 

Lissu alikamatwa juzi jijini Dar es Salaam, akiwa maeneo ya mahakama hiyo ya Kisutu, akituhumiwa kwa madai ya kumkashifu rais wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari  kwenye hoteli ya Protea siku chache zilizopita.

Siku ya mkutano huo, Lissu aliibua sakata linalohusu Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd(SCEL), kuishikilia Ndege ya Bombardier Dash 8 nchini Kanada,hadi itakapolipwa deni lake la Sh87bilioni.

No comments