Breaking News

Mbunge Chadema amuunga mkono Magufuli

MBUNGE wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka amesema mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme katika bonde la Mto Rufiji ambao Rais John Magufuli amesema ni lazima ufanyike lije jua au mvua, utaokoa fedha ambazo serikali imekuwa ikigharamia umeme wa mafuta.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalumu juzi, Kaboyoka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema nchi inapotaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda, umeme wa dizeli au petroli, kwa kuwa ni wa gharama kubwa, hufifisha mkakati huo.

Akizungumza jijini juzi, Rais Magufuli alisema ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) mkoani Pwani lazima ufanyike.

Rais alikuwa akizungumza katika ufunguzi wa Maonyesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), Manispaa ya Temeke.

Aliwaeleza wawekezaji kuwa changamoto ya umeme wa uhakika itakwisha kupitia bwawa hilo, kwani nchi itakuwa na umeme wa jumla ya megawati mpaka 5,000 utakapokamilika mradi huo.

“Inyeshe mvua, liwake jua Stiegler’s Gorge itajengwa," alisema Rais Magufuli kwa sababu "tumeamua kuchukua juhudi za makusudi kuifufua na ninawahakikishia wawekezaji tunaifufua...

"Na tunaanza kwa fedha yetu.”

GHARAMA NAFUU

Mama Kaboyoka alisema umeme wa maji ndiyo wa gharama nafuu zaidi duniani na kwamba nchi itanufaika zaidi kwa kuwa mradi huo utatoa umeme mwingi kwa gharama nafuu.

“Ingekuwa ni kuchimba madini hapo ningesema kutakuwa na uharibifu, lakini kutegeshea kujenga mitambo ya maji na mazingira mtu yeyote ukitengeneza maji utalinda na mazingira yako kwa kuweka miti,”alisema Kaboyoka akizungumzia maoni ya wanaharakati kuwa ujenzi huo utaharibu mazingira.

Aliuliza bwawa la Kidatu mkoani Tanga lenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 200, kwa mfano, limeharibu mazingira gani?

Alisema ni vyema kuangalia maoni ya wanaharakati huwa ni kwa faida ya nani, hasa baada ya mradi huo kuwa 'kizobo' cha mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma kupitia mikataba ya ununuzi wa umeme wa dharura.

“Kinachotakiwa ni kuwachukulia hatua kwanza hawa waliotuingiza kwenye mikataba mibovu," alisema zaidi Kaboyoka.

"Huwezi kununua umeme kutoka IPTL kwa zaidi ya Sh. 520 halafu wewe ukauze kwa bei nafuu... yaani unakwenda sokoni kununua mahindi debe moja kwa Sh. 5,000 halafu unakwenda kuuza kwa Sh.2,000. Hivi kweli ni akili hiyo?”

Ujenzi wa bwawa hilo katika Mto Rufiji unatarajiwa kufanywa na wataalamu kutoka Ethopia.

“Miaka 10 ijayo umeme utakaotokana na maji hayo utakuwa mkubwa sana, ina maana nchi yetu itaweza kupata nishati ya kutosha kwa viwanda vyake."

No comments