Breaking News

Mbowe amuunga mkono Zitto


Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akichangia kuhusu miswada mitatu inayohusu rasilimali za nchi bungeni mjini Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman 

Kwa ufupi

Asema kati ya miswada mitatu waliyonayo, mabadiliko ya sheria ya madini ndiyo mkubwa zaidi yanaohitaji ushirikiano wao.

By Julius Mnganga, Mwananchi jmathias@mwananchi.co.tz

Dodoma. Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe ameunga mkono msimamo wa Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kuhusu miswada inayojadiliwa hivi sasa kwamba mfumo wa uzalishaji madini kuendelea kubaki uleule ni suala litakaloleta shida huko mbele.

 “Zitto amezungumza, kwamba tuna asilimia 25 kwenye mgodi wa Mwadui lakini hatunufaiki chochote na mgodi huo. Kuwa na hisa hakusaidii kama husimamii uzalishaji,” amesema Mbowe.

Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, amebainisha hilo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma akiwaongoza wabunge wa wanaotoka vyama vinavyounda Ukawa walipokuwa wakieleza kutokubaliana na namna mabadiliko ya sheria hasa ya madini inavyofanywa.

Aliwatahadharisha kwamba kurushiana maneno kunawapotezea muda muhimu walionao kukamilisha kazi hiyo na kuwakumbusha kwamba, kati ya miswada mitatu waliyonayo, mabadiliko ya sheria ya madini ndiyo mkubwa zaidi yanaohitaji ushirikiano wao.

Akizungumzia msimamo wao, (Ukawa) Mbowe alisema muda uliotolewa kwa ajili ya maandalizi ya mjadala wa miswada hiyo hautoshi kulingana na unyeti wake. Alikumbusha kwamba, mara nyingi, Serikali imekuwa ikitumia hati za dharura kupitisha malengo yake.

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alitahadharisha kuwa kilichotokea Zimbabwe mwaka 2002 kinaweza kutokea nchini siku za mbele kutokana na mabadiliko hayo.

“Wapinzani wa Zimbabwe walipotahadharisha kuhusu mabadiliko yaliyokuwa yanafanywa, waliitwa watetezi wa wazungu lakini leo hii nchi hiyo haina sarafu. Bunge letu linafanya kama Zimbabwe bila kujali kuwa tulipelekwa huko kwenda kujifunza,” alisema Mbatia.

No comments