Matumaini mapya, bei ya dawa yashushwa
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kupungua kwa bei ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kutokana na Serikali kuzinunua moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa (MSD), Laurean Bwanakunu. Picha na Omar Fungo
DONDOO
>>Bei ya dawa inatakiwa kuongezeka kwa asilimia 3 hadi asilimia 10 kwa bei iliyonunuliwa katika duka la MSD
>>Sh269 bilioni ni Bajeti ya Serikali kwa ajili ya dawa na chanjo kwa mwaka 2017/2018
Dar es Salaam. Ukipata ugonjwa wa aina yoyote, kuna mambo mengi huwa unafikiria. Mmoja ya mambo hayo ni gharama ya dawa kutibu ugonjwa ulionao.
Serikali imeliona hilo, na sasa kuna habari nzuri. Bei ya dawa inakwenda kushuka.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Novemba 2015 kuitaka Bohari ya Dawa (MSD) kununua dawa na vifaatiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji na si madalali.
Licha ya hilo, Serikali inakusudia kuunda mamlaka ya udhibiti wa bei za dawa za binadamu na vifaatiba ambayo mmoja ya kazi zake itakuwa kupanga bei elekezi ya dawa.
Mwalimu alisema Serikali itaanza kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya washitiri (watu wa kati) ili kupunguza gharama kwa Serikali na hilo litafanya gharama za manunuzi ya dawa kupungua kwa kati ya asilimia 15 hadi 80.
Mfano dawa ya kupambana na maambukizi ya bakteria (Amoxicillin 625 mg) awali ilikuwa inauzwa Sh 9,800 lakini sasa itauzwa 4,000, shuka moja lililokuwa likiuzwa Sh22,200 sasa litauzwa 11,100 na boksi la grovusi lililokuwa likiuzwa Sh19,200 sasa litauzwa kwa Sh18,200.
Baada ya kuwasilisha taarifa yake kwa vyombo vya habari Waziri Mwalimu ambaye pia ana dhamana ya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, aliruhusu maswali ya waandishi wa habari ndipo akaulizwa juu ya mpango wa Serikali wa kuhakikisha bei ya dawa haimuumizi mlaji wa mwisho kama inavyoelekezwa na MSD. Alikuwa na majibu.
“Tunaandaa na tunakusudia kuwa na ‘Ewura’ (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji) lakini hiyo itakuwa ni kwa ajili ya kudhibiti bei na ubora wa dawa kwani unakuta bei ya dawa MSD inafahamika, lakini wamiliki wa maduka binafsi ya dawa wanauza kwa bei ya juu karibia asilimia 100 zaidi. Katika hospitali binafsi kuna bei kubwa kuliko uhalisia,” alisema Waziri Mwalimu.
Alisema mpango huo haukusudii kuyaua maduka binafsi ya dawa ila unalenga kupunguza mzigo wa gharama kwa mlaji wa mwisho na kuhakikisha mwananchi wa chini anakuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Awali akizungumzia utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, Waziri Mwalimu alisema MSD imeingia mikataba ya miaka miwili na wazalishaji 73 wa dawa muhimu na kati yao 10 ni wa hapa nchini na kwa ujumla wana uwezo wa kuzalisha dawa 178 za aina tofauti na vifaa tiba 195.
Itakumbukwa kuwa wakati wa hotuba ya kutimiza mwaka moja madarakani, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Wizara ya Afya kuhakikisha MSD wanabadili mfumo wao wa manunuzi ya dawa kwa kuacha kuwatumia madalali na mawakala na badala yake idara hiyo ianze kufanya manunuzi kutoka kwa wazalishaji.
“Sasa msimamo na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji bila kupitia kwa washiriti, hivyo kupunguza gharama za Serikali… hadi sasa MSD imeingia mikataba na wazalishaji 73 ambao kati yao 10 ni wa ndani,” alisema Mwalimu.
Alisema Wizara ya Afya inaunga mkono jitihada za Rais kujenga uchumi wa viwanda na si kwamba dawa zinazonunuliwa nchini hazina ubora, ubora zinao unaohitajika na zimethibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
“Sekta ya afya tumefanya maamuzi ya makusudi kuunga mkono juhudi za kuimarisha uchumi wa viwanda kwani baadhi ya dawa tunazozinunua kwa wazalishaji wa ndani bei zake ni ghali kuliko zikiagizwa nje ya nchi, lakini uzuri wa hizi dawa usambazaji wake ni wa haraka tofauti na za kuagiza ambazo huchukua hadi miezi mitatu hadi sita,” alisema Mwalimu.
Alisema utaratibu huo mpya utasaidia upatikanaji wa dawa muhimu kwa asilimia 90 na utapunguza gharama za manunuzi ya dawa kwa kati ya asilimia 15 hadi asilimia 80. Alitolea mfano dawa ya homa ya ini ambayo awali ilikuwa inauzwa Sh22,000 ambayo sasa itauzwa Sh5,300.
Alitoa maelekezo kuwa hospitali zote, zahanati na vituo vya afya vya Serikali kuwa vinapaswa kushusha bei ya dawa kwa sababu bei hiyo imeanza kutumika tangu Julai Mosi, hivyo akawaagiza wakurugenzi wa halmashauri kusimamia suala la dawa na kupeleka mahitaji sahihi ya dawa katika maeneo yao na kwa wakati.
Alisema tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Afya changamoto kubwa aliyoikuta ilikuwa ni suala la upungufu wa dawa kutokana na changamoto za rasilimali fedha za kutosha, lakini Rais ameongeza fungu na sasa hali inaridhisha na ndio maana ameitaka MSD kuongeza idadi ya dawa muhimu kufikia walau 300.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema miongoni mwa matunda ya utumiaji utaratibu huo mpya wa manunuzi vituo vya afya na hospitali vitakuwa na uwezo mkubwa na kununua dawa nyingi na kwa fungu dogo kutokana na kushuka kwa bei.
“Bei ya dawa itapungua na watoa huduma wataongeza uwezo wao wa kununua dawa nyingi kwa bajeti ndogo, hata wananchi watauona unafuu huo katika huduma za afya. Waziri anasema upatikanaji wa dawa muhimu utafikia asilimia 90, lakini huenda ukafika asilimia 100 endapo halmashauri zitakuwa zinawasilisha mahitaji halisi ya maeneo yao,” alisema Bwanakunu.
Aliongeza kuwa bei mpya ya dawa hizo utatangazwa kwa wananchi na itasambazwa kupitia katika kitabu cha mwongozo wa bei mpya za dawa na tovuti yao ili kila mwananchi aweze kufahamu.
No comments