Breaking News

Likizo ya hakimu yasababisha kesi dhidi ya akina Lissu kuahirishwa


Washitakiwa wanadaiwa kuandika habari ambayo iliwatisha wananchi wa Zanzibar wasishiriki katika uchaguzi wa marudio.

Kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wahariri wa gazeti la Mawio imeahirishwa hadi Agosti 7 kwa sababu Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba anayeisikiliza yupo likizo.

Shauri hilo leo (Julai 5) limeahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.

Washtakiwa waliwakilishwa mahakamani na wakili Nashon Nkungu, huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Said Hamis.

Washtakiwa wengine ni wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume cha Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Wanadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, Idrisa, Mkina na Lissu waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, Machafuko yaja Zanzibar.

Pia wanadaiwa Januari 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala,  Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Anadaiwa alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa marudio.

No comments