HIVI NDIVYO WATANZANI 24 WALIVYOTEKWA NA WAASI HUKO CONGO
Dar es Salaam. Baadhi ya madereva 24 waliotekwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wameelezea jinsi walivyotekwa hadi kufanikiwa kurudi nchini salama.
Madereva waliotekwa walikuwa 24, kati yao 21 Watanzania na watatu ni raia wa Kenya.
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa madereva hao, Rajabu Msonzo alisema walitekwa Juni 29 saa 11 asubuhi wakati wakiwa wameshaingia Congo, kijiji cha Baraka.
“Tuliondoka nchini Juni 17, tukafika Congo Juni 24, wakati huo tulikuwa tumeshasimama katika kijiji cha Uvira kwa ajili ya kukaguliwa na kupewa askari ambao watatulinda safarini,” alisema.
Msonzo alisema Juni 29 waliwasili katika kijiji cha Lulimba ambapo walilazimika kulala hapo huku wakiwa katika uangalizi wa askari waliotoka nao mpakani.
“Lakini, ilipofika saa 11 asubuhi, tulisikia milio ya risasi tulipoegesha malori huku tukiwa ndani tumelala. Askari waliokuwa wametusindikiza walijibu mapigo, lakini walizidiwa nguvu,” alisema.
Msonzo alisema waasi hao hawakuwa na nia ya kuwadhuru bali walilenga kuwadhibiti wanajeshi waliokuwa katika kambi iliyokuwa kijiji cha jirani.
Alisema shida kubwa ya waasi hao ilikuwa ni kuteka kambi ya jeshi ambayo ilikuwa karibu na eneo walilokuwa wameegesha magari yao.
Msonzo alisema waasi hao walifanikiwa kuwasambaratisha wanajeshi wa Congo.
“Walipofika katika magari yetu walituuliza sisi ni nani na mbona tunatembea na wanajeshi wa Serikali ya Congo. Pia, walitwambia sisi ni wezi tunashirikiana na viongozi kuwaibia watu wa Congo, waasi hao walikuwa kama 100 ,” alieleza Msonzo.
Baada ya waasi kufanikiwa kuwashambulia wanajeshi katika kambi hiyo waliwashurutisha wananchi na kuwalazimisha kuingia ndani ya kambi hiyo wawasaidie kubeba silaha.
Msonzo alisema waliwanyang’anya chakula, pesa na maji katika magari yao yote 24 huku wakitishia kuwaua. Hata hivyo, fedha walizonyang’anya ni zile zilizokuwa kwenye magari na si za mfukoni mwao.
“Wenzetu wengine walikuwa wakipigwa vibao na kulazimishwa kusema ukweli kwa kuwa walidhani sisi tunashirikiana na viongozi wa jeshi la DRC,” alisimulia.
Baada ya hapo, waasi hao waliwapeleka madereva hao katika chumba kidogo ambacho kilikuwa kikitumika kama sehemu ya biashara.
“Hakukuwa na chochote na hivyo tulilazimika kuweka maboksi na kulala,” alisema.
Alisema kwa kuwa waasi hawakuchukua simu zao, walifanikiwa kuwapa taarifa ndugu na jamaa walioko Tanzania kuhusu kilichowasibu Congo.
“Muda mfupi baada ya kuwasiliana na uongozi wa Tanzania na kampuni zilizotuajiri, tulishuhudia ndege za Umoja wa Mataifa zikizunguka eneo lile bila kujua nini hatma yetu,” alisema.
Msonzo alisema hadi kufikia Julai 4 waasi hao walipungua idadi, baada ya kupata taarifa kuwa Jeshi la Congo linakuja katika eneo hilo.
“Kwa bahati nzuri dereva mwenzetu aliondoka kwa kudandia magari yaliyokuwa yamewapakiza wananchi wakielekea mpakani katika kijiji cha Baraka. Alipofika huko alitupa taarifa kuwa watu wanapita na waasi hawapo,” alisema.
Alisema waliposikia kuwa hali ni shwari mpakani waliamua kuondoka na malori yao na kuyaacha mengine, wakaelekea mpakani, katika kijiji cha Baraka.
Msonzo alisema Julai 6 walifanikiwa kulala mpakani mwa Rwanda na Congo na ilipofika Julai 8 walianza safari ya kurudi nchini.
Akizungumzia kurudi salama kwa madereva hao, Naibu Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Susan Kolimba alisema Serikali ilihakikisha madereva hao wanarudi salama.
Kabla ya madereva hao kurejea wizara hiyo ilitoa waraka ukisema madereva hao 24 walitekwa Congo na kikundi cha waasi cha Maimai.
No comments