Breaking News

Dida ahamishia majeshi Sauz

Kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’, rasmi anaondoka kwenye timu hiyo baada ya kufanikiwa kufuzu majaribio katika Klabu ya University of Pretoria ya Afrika Kusini ‘Sauz’. 

Dida atasaini kuichezea klabu hiyo kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita wa ligi kuu. 

Kuondoka kwa kipa huyo, kunabakiza makipa watatu ambao ni Beno Kakolanya na Ally Mustapha ‘Barthez’ anayedaiwa kwenda Singida United hivi karibuni na Rostand Youthe aliyesajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu. 

Kipa huyo juzi asubuhi aliomba kufanya mazoezi ya gym ya pamoja ya Yanga kwa ajili ya kujiimarisha kabla ya kwenda kujiunga na timu hiyo. 

Mtoa taarifa huyo alisema, kipa huyo baada ya kufuzu majaribio hayo, atakwenda kusaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea University of Pretoria ya nchini huko. 

Alipotafutwa Dida kuzungumzia hilo alisema: “Kwa hivi sasa siwezi kuzungumza vizuri kwani ninaendesha gari, hivyo kwa kuhofia ajali barabarani ninaomba nipigie baadaye.” 

Meneja Mkuu wa Yanga, Hafidh Saleh alipotafutwa kuzungumzia suala la kipa huyo kufanya mazoezi na timu hiyo, alisema: “Ni kweli Dida alifanya mazoezi ya gym na timu, ni baada ya kuomba kujiandaa kabla ya kwenda kujiunga na timu aliyofuzu majaribio nchini Sauz." 

No comments