Daraja la mto Kilombero lafungwa kupisha ujenzi
Wakazi wa wilayani Kilombero wanatarajia kurejea katika matumizi ya kivuko katika kuvuka mto Kilombero kufuatia daraja la mto Kilombero linalounganisha wilaya za Ulanga na Malinyi kufungwa kwa muda.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Meneja wa Wakala wa Barabara mkoani Morogoro, Mhandisi Dorothy Mtenga alisema Daraja hilo litafungwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Julai 4 ili kupisha uwekaji wa lami katika matuta ya daraja hilo.
“Ni kweli tutalifunga daraja lwa mto Kilombero kwa muda wa mwezi mmoja ili kupisha mkandarasi aweze kuweka lami katika matuta ya daraja, ujenzi ulisimama kupisha mvua za masika,” alisema meneja huyo.
Aliwataka wananchi wa wilaya za Kilombero na Malinyi kuwa wavumilivu na kuendelea kutumia kivuka kwa kipindi cha mwezi mmoja ili kupisha ujenzi wa daraja hilo ukamilike katika ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo aliwataka wakandarasi wa daraja hilo wajitahidi ili kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kuwaepushia wananchi kero ya kutumia kivuko.
Ihunyo alisema tayari wananchi wameshafahamishwa kuwa watalazimika kuendelea kutumia kivuko kwa kipindi cha mwezi mmoja ili kupisha ujenzi huo ambao umefikia katika hatua za umaliziaji.
No comments