Ajibu kupelekwa hospitali kwanza
Kocha wa timu hiyo, George Lwandamina.
MUDA mfupi baada ya Yanga kumtambulisha mshambuliaji, Ibrahim Ajibu aliyetokea Simba, kocha wa timu hiyo, George Lwandamina ameagiza mchezaji huyo apelekwe hospitali kupimwa afya yake.
Yanga imemsajili Ajibu kwa mkataba wa miaka miwili akiwa ametoka kumaliza mkataba wake na Simba kwa dau la Sh milioni 50.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema wataenda na Ajibu hospitalini kwa ajili ya kumpima afya kabla ya kuanza kambi ya timu hiyo.
“Kocha ametoa agizo la kuhakikisha tunampima Ajibu afya kabla ya kuanza maandalizi yetu kwa sababu anataka kufahamu ni mchezaji gani ambaye hataweza kumudu mazoezi yake muda mfupi baada ya kuanza kambi.
“Lakini zoezi hilo pia litafanyika kwa wachezaji wote ikiwemo Abdallah Shaibu (Ninja) tuliyemsajili hivi karibuni kutoka Zanzibar, pia wachezaji wote nao watapimwa afya zao,” alisema Hafidh.
Alisema Lwandamina ameweka utaratibu huo ili kujua mapema afya za wachezaji wake kabla ya kuanza kambi ya mazoezi kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Jana Ijumaa baadhi ya wachezaji wa Yanga akiwemo Amissi Tambwe walipimwa afya zao kutekeleza agizo hili la Lwandamina lakini Ajibu yeye anapimwa leo na nyota wengine wa timu hiyo.
No comments