Breaking News

Yanga uso kwa uso na Wakorea leo

TIMU ya soka ya vijana ya Yanga leo watashuka kwenye Uwanja wa Uhuru kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Halelujah kutoka nchini Korea. 

Mchezo huo utakaoanza majira ya saa 8:00 mchana na kujumuisha matukio mbalimbali ya kimichezo kwa watoto, imeandaliwa na Kanisa la TAG. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Mbezi A, Huruma Nkone, alisema mashabiki na watu waote watashuhudia mchezo huo bure wakiwa na lengo la kutoa burudani kwa watu wote bila kujali madhehebu na dini zao. 

Mchungaji Nkone alisema lengo la mechi hiyo ni kudumisha umoja mshikamano na upendo kati ya nchi ya Korea na Tanzania na kuwapa burudani wananchi. 

Alisema maandalizi ya mechi hiyo ya kirafiki yamekamilika na tayari Wakorea hao wamewasili nchini juzi huku wakiahidi kuonyesha kandanda la kuvutia. 

"Mbali na soka, kutakuwa na programu mbalimbali zitakazokuwa zikiendelea na michezo ya kuvutia kwa ajili ya watoto, kwa kweli si ya kukosa wote,", alisema mchungaji Nkone. 

Alisema pia kutakuwa na burudani za nyimbo za dini kutoka kwa wasanii na vikundi mbalimbali vya nyimbo za dini pamoja na waimbaji kutoka Korea.

No comments