Mtoto achomwa mikono akidaiwa kuiba Sh7,000
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika Hospitali ya Kinyonga wilayani Kilwa jana (Ijumaa) alipolazwa mtoto huyo, mama yake alisema kuwa alichukua uamuzi wa kumchoma moto mtoto huyo kutokana na kuchoshwa na tabia yake ya wizi na mashtaka ya kuwa na tabia ya udokozi wa mara kwa mara.
Kilwa. Mtoto Razaki Ali (9) wa Kijiji cha Miramba wilayani Kilwa mkoani Lindi amechomwa moto mikononi na mama yake mzazi, Zabibu Binamu kwa madai ya kuiba Sh7,000.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika Hospitali ya Kinyonga wilayani Kilwa jana (Ijumaa) alipolazwa mtoto huyo, mama yake alisema kuwa alichukua uamuzi wa kumchoma moto mtoto huyo kutokana na kuchoshwa na tabia yake ya wizi na mashtaka ya kuwa na tabia ya udokozi wa mara kwa mara.
Zabibu alisema alimchoma moto mikononi mtoto huyo baada ya kuiba Sh7, 000.
“Jamani naomba niwaeleze kisa na mkasa kwa ujumla mtoto huyo amekuwa na tabia ya wizi na udokozi wa mara nyingi hivyo niliamua kumchoma ili kukomesha tabia hiyo,” alisema zabibu.
Zabibu alisema baada ya kumchoma moto hakumkupeleka hospitali na badala yake alimpaka asali.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kinyonga Wilaya ya Kilwa, Saleh Abubakari alisema mtoto huyo ameungua vibaya na hata akipona huenda akawa mlemavu.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Renata Mzinga alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kueleza kuwa mama amemchoma moto mwanaye kwa kumfunga na majani makavu na kumsababishia maumivu na majeraha mikononi.
“Mama wa mtoto anashikiliwa na jeshi, lakini kwa sasa yuko nje kwa dhamana na taratibu nyingine za kisheria zinaendelea,” amesema.
Mwanaharusi Hamisi Kumala jirani wa mtoto huyo alisema siku ya tukio Razaki alikimbilia kwake kuomba msaada baada ya mama yake kumchoma moto kwa madai ya kuiba fedha hizo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wilaya ya Kilwa, Tumainieli Mpunga ameiomba Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wazazi na walezi wenye tabia ya ukatili dhidi ya watoto.
No comments