Breaking News

Maghembe aiambia Uingereza kuna utakatishaji fedha kwenye mifugo

Wakati operesheni hizo zikiendelea, Serikali imesema imebaini mchezo unaofanywa na wafanyabiashara haramu wakiwamo majangili kutumia mbinu za kutakatisha fedha kwa kununua makundi ya mifugo, kuyachunga kwenye maeneo ya hifadhi nchini na baadaye kuuza kwa faida kubwa minadani

Huku kukiwa na operesheni kadhaa zinazoendelea katika maeneo ya hifadhi za misitu na mapori ya akiba kuwaondoa wafugaji waliovamia sehemu hizo, uhalifu mwingine unaohusiana na uingizaji mifugo umebainika.

Operesheni mbalimbali zinaendelea kuwaondoa wafugaji katika msitu wa Burigi mkoani Kagera na pori la Buhindi wilayani Sengerema.

Wakati operesheni hizo zikiendelea, Serikali imesema imebaini mchezo unaofanywa na wafanyabiashara haramu wakiwamo majangili kutumia mbinu za kutakatisha fedha kwa kununua makundi ya mifugo, kuyachunga kwenye maeneo ya hifadhi nchini na baadaye kuuza kwa faida kubwa minadani.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema hayo alipozungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Taarifa ya wizara hiyo ilimkariri Profesa Maghembe akisema Serikali imebaini ujanja huo na sasa inajipanga namna ya kushughulika na wahalifu hao ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimeifikisha nchi kwenye migogoro ya ardhi, huku mifugo hiyo ikiharibu maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji.

“Wanapoingiza mifugo ndani ya hifadhi, huingia na majangili na wachoma mkaa. Tumebaini pia kuwa karibu nusu ya mkaa unaovunwa Tanzania huuzwa nje ya nchi na hasa za jirani, hatutakubali vitendo hivyo viendelee ni lazima misitu yetu iliyobakia ilindwe na kuhakikisha kuwa inaendelea kuwapo,” alisema waziri huyo

Akizungumzia athari za kimazingira zitokanazo na uharibifu wa misitu, Profesa Maghembe alisema kwa sasa maeneo mengi nchini yaliyokuwa yakipata mvua kwa miezi mitano mfululizo yamekuwa yakipata chini ya kiwango na kufikia kati ya miezi mitatu au miwili hali inayotishia nchi kuwa jangwa.

Balozi Cooke alimhakikishia Waziri Maghembe kuwa atakuwa mwakilishi mzuri wa vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Uingereza na kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili katika sekta ya uhifadhi.

Pia, aliahidi kuwashawishi wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza Tanzania katika sekta ya uhifadhi na utalii ili kuchangia katika ukuaji wa pato la Watanzania.

No comments