Breaking News

JPM:SASA WANAANZA KUNYOOKA


RAIS John Magufuli amesema anawachukia wezi wa rasilimali za nchi na kwamba tayari amekwishawanyoosha baadhi yao na anaendelea kuwakomesha wengine, kwa sababu ndio walioliingiza taifa katika umasikini.

Aidha, Rais amesema katika kuhakikisha kunakuwa na umeme wa kutosha kuendesha nchi ya viwanda, serikali itajenga bwawa kubwa la kuzalisha nishati hiyo katika maporomoko ya maji ya Stieglers Gorge yaliyoko kwenye Mto Rufiji ndani ya Pori la Akiba la Selous.

Alisema hayo jana katika viwanja vya Bwawani wilayani Kibaha mkoani Pwani akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi ya siku tatu, iliyolenga kuzindua viwanda vitano pamoja na kuzungumza na wananchi. Alisema Mungu hakuwaletea Watanzania umasikini kwa sababu ni nchi yao, ina rasilimali nyingi yakiwemo madini na vivutio vinavyoifanya ionekane ni tajiri.

Hata hivyo, alisema watu wake wanaishi katika hali ya umasikini kutokana na wizi wa wachache wasio waaminifu, wakiwemo baadhi ya watumishi walioaminiwa na umma, lakini wakageuka na kusaliti taifa. Aliwaomba Watanzania kumwombea kwa kuwa ameasisi vita ngumu itakayoumiza wachache, ili kunufaisha wengi. “Watanzania niombeeni kwa kuwa nimeanzisha vita itakayoumiza wachache ili wengi wanufaike.

Hii ni vita kwa sababu itaumiza baadhi ya watu. Niombeeni kwa Mungu niishinde kwa faida yetu sote. Nachukia wezi na nitalala nao sambamba mpaka wakome na waione dunia ilivyo kwa kuwa wametufanya maskini,” alisema. Akaongeza, “Mimi nachukia wezi, na kwa kweli wezi watakoma tu, awe mwizi wa Tanzania, awe mwizi wa Ulaya, awe anatoka Magharibi, Mashariki, Kaskazini au Kusini, mwizi ni mwizi tu.”

Rais alisisitiza kuwa, baadhi ya watu walioliingiza Taifa katika umaskini kwa makusudi, ameanza kuwashughulikia na wengine wameanza kunyooka. Aliwatahadharisha waliopo serikalini kufanya kazi kiuadilifu ili wasiwepo wanaoendelea kulisababishia taifa upotevu wa rasilimali akisema, hatawaacha waendelee kuliibia taifa, kwa sababu alichaguliwa na Watanzania ili atetee maslahi ya wote, wakiwemo wanyonge.

Alizungumzia ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme na kusema kuwa pamoja na kupanua mradi wa umeme wa Kinyerezi 1, 2 na 3 ili nchi iwe na nishati hiyo ya kutosha, watawatumia wataalamu waliojenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme Ethiopia ili wajenga kama hilo nchini. Asifu uongozi Pwani Rais alionesha kufurahishwa na uongozi wote wa Mkoa wa Pwani kuanzia Mkuu wa Mkoa hadi ngazi za chini kwa jitihada uliozionesha kuhakikisha uanzishaji wa viwanda unashika kasi, huku vingine vikikamilika tayari kwa kuzinduliwa na vingine vikiwa katika hatua mbalimbali za maendeleo.

Alisema, “Bila kutia unafiki, ninasema wazi kuwa viongozi wa mkoa huu wa Pwani wamenifurahisha kwa kuhakikisha viwanda vinaanzishwa kwa kasi. Nimefurahi kuona Pwani ikiwa na viwanda 371 kati ya hivyo vikubwa ni 89, vya kati na vidogo vitakavyozalisha ajira nyingi nchini vikiwa ni zaidi ya 260.” Alisema akiamua kuzungukia viwanda vyote vya mkoani humo ili kuvizindua, itamlazimu kutumia mwezi mzima kwa sababu ndio mkoa unaoongoza kwa kuanzisha viwanda vingi vikubwa.

Alihoji kulikoni mikoa yenye malighafi kama vile chuma haina kiwanda hata cha misumari wakati Mkoa wa Pwani usiochimba chuma una kiwanda kikubwa cha bidhaa hiyo. Kutokana na hilo, Rais aliwataka viongozi wa mikoa isiyo na viwanda wajitathmini na kujihoji ni kwa namna gani wanasaidia kunyanyua maisha ya wanyonge kwenye maeneo yao ikiwa hawajaweza kuchochea uanzishwaji wa viwanda vitakavyowatengenezea ajira.

Alisisitiza kuwa lengo lake ni kuwainua Watanzania masikini kutoka walipo kwenda kwenye hatua nyingine ya maendeleo, hivyo katika awamu ya uongozi wake anataka kuwa na viongozi watakaomsaidia kufanikisha azma hiyo na si vinginevyo. Mkuu wa nchi aliwataka viongozi wasioweza kuendana na kasi yake wajitathmini na kujiondoa wenyewe mapema, badala ya kusubiri awaondoe, kwa sababu hatasita kufanya hivyo kwa atakayeona kuzorotesha maendeleo.

Bei za bidhaa Kwa mujibu wa Rais, uwepo wa viwanda vingi nchini, vikiwemo vya nguo na vya bidhaa nyingine utasaidia kushusha bei za vitu na kuwafanya Watanzania wa hali ya chini kumudu maisha na kuyafikia yaliyo bora. “Tuanzishe na kuimarisha viwanda vyetu ili hata nguo tutengeneze sisi na kuwauzia Wazungu mitumba. Tusitegemee viwanda vya nje.

Tukiwa na vyetu Watanzania watapata kazi na pato la taifa litazidi kukua. Hili ndilo lengo langu tangu mwanzo nilipogombea Urais, nipeni ushirikiano ili nilitekeleze,” alisema Rais. Umeme na maji Akijibu maombi ya Mbunge wa Kibaha Mjini, Sylvestry Koka (CCM) aliyemweleza kuhusu changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji na umeme wa uhakika unaoendana na uwepo wa viwanda vingi mkoani humo, Rais Magufuli alisema serikali inaendelea kutekeleza ahadi zake hatua kwa hatua kuhakikisha changamoto hizo zinakwisha.

Alimhakikishia mbunge huyo na wana Kibaha kuwa umeme unaosambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) hadi kufikia mwaka 2019 utakuwa umekwisha unganishwa kwenye vijiji 204 vya mkoa huo na kwamba vijiji vingine 127, navyo vitakuwa vimekwishafikishiwa huduma hiyo ifikapo mwaka 2020. Rais alisema tayari mradi wa REA III umekwishaanza na kwamba Sh bilioni 30.2 zitahusika katika mradi huo.

Alieleza masikitiko yake kuhusu matapeli katika miradi mbalimbali na kusema kuwa, mradi wa umeme ni miongoni mwa inayoingiliwa na watu hao wasio waaminifu, hivyo kuhitaji umakini wa hali ya juu. Kuhusu maji, alisema leo atazindua mradi wa maji wa Ruvu, utakaohudumia miji ya Bagamoyo, Dar es Salaam na Kibaha. Rais alisema litajenjwa bwawa la Kidunda litakalohifadhi maji ya mvua yatakayotumika wakati wa kiangazi.

Alionya wananchi wa maeneo hayo wasiache maeneo yakawa na majani marefu badala ya kupanda vyakula kwa sababu watakapolia njaa na kuitaka Serikali iwaletee chakula, atawaambia kuwa hakuna chakula ili wachague mahali pengine pa kukipata. “Wakati huu mvua zinaponyesha msiache kulima hata kama ni maharage au mboga ili msije mkalia njaa kwa kuwa sitakuwa na cha kuwapa. Tumieni maeneo yenu vizuri yasibaki kuwa mapori,” alisema.

Afya Aliweka wazi mipango ya serikali kuendeleza sekta ya afya mkoani Pwani na kusema kuwa, mwaka huu vitanunuliwa vitanda vya kulaza wagonjwa 3,680 kwa ajili ya hospitali mkoani humo, vingine 920 kwa ajili ya kujifungulia, magodoro 5,000 na mashuka 10,000 na kwamba Sh bilioni 2.93 zitatumika. Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisisitiza kuwa, wananchi wa Mkoa wa Pwani hawana budi kushirikiana kufichua uhalifu ili kuyafanya maeneo yao kuwa salama na ya kuvutia zaidi kwa uwekezaji.

Alikiri mafanikio katika mfumo wa elimu bure ambapo wanafunzi katika shule za sekondari na msingi walioandikishwa waliongezeka maradufu. Alisema mkandarasi wa kujenga bandari kavu wilayani Kibaha amekwishapatikana na kwamba ujenzi utaanza ili ukikamilika mizigo yote inayotoka katika bandari ya majini ichukuliwe kutoka katika bandari hiyo.

No comments