Breaking News

JPM atoa vifaa tiba vya Sh16 milioni jimboni kwa Ridhiwani Kikwete

Rais John Magufuli 

Vifaa hivyo yakiwamo magodoro 20 na mashuka 50 vitatumika katika vituo vya afya na zahanati zilizopo ndani ya halmashauri hiyo.

Pwani. Raisi John Magufuli ametoa msaada wa vifaa vya afya vyenye thamani ya zaidi ya Sh16milioni kwa Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani.

Vifaa hivyo yakiwamo magodoro 20 na mashuka 50 vitatumika katika vituo vya afya na zahanati zilizopo ndani ya halmashauri hiyo.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amekabidhi vifaa hivyo kwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Maria Moreto.

Akikabidhi vifaa hivyo leo,(Ijumaa)Ridhiwani amesema Rais aliamua kutoa vifaa hivyo baada ya kutambua changamoto zinazoikabili Idara ya Afya ndani ya Halmashauri hiyo.

"Hivi vifaa vimetolewa na Rais wetu kwa kuwa anatambua umuhimu wa kuboresha huduma na mahitaji ya wananchi wake, hivyo ni jambo la kushukuru,"amesema.

Ridhiwani amesema kuwa ingawa changamoto zipo nyingi kwenye Idara ya Afya lakini Serikali kuu kwa kushirikiana na bajeti ya halmashauri hiyo wamekuwa wakiendelea kuzipunguza siku hadi siku kadri fedha zinavyopatikana.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Maria Moreto amesema vifaa hivyo vya tiba ni faraja kwa wakazi wa Chalinze hususan kwa upande wa wanaojifungua.

"Kwa niaba ya halmashauri nichukue fursa hii kumshukuru Raisi wetu mpendwa kwa kutuona sisi wakazi wa Chalinze na kutupatia msaada huu na sisi tunamuahidi kuwa tuko pamoja katika kukabiliana na changamoto hizi, "amesema.

Diwani wa Viti Maalumu kutoka Halmashauri hiyo Mwanakesi Madega amesema kuwa kutokana na majukumu waliyonayo watahakikisha vifaa hivyo vinasambazwa kulingana na mahitaji kwenye zahanati na vituo vya afya ili vitumike kama inavyostahili.

No comments