Waziri Makamba Awatoa Hofu Watanzania mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge
Baada
ya mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge katika Pori la Akiba la Hifadhi
ya Selous kutikisa Bunge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais (Muungano
na Mazingira), January Makamba amewataka Watanzania kutulia na
kubainisha kuwa tathmini ya mradi huo inafanyika.
Makamba
ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 23, 2018 wakati akihojiwa katika
kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Redio Clouds.
Jana
bungeni mjini Dodoma mradi huo ulikuwa gumzo wakati wabunge wakijadili
bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka wa fedha 2018/19,
ambapo baadhi ya wawakilishi hao wa wananchi akiwemo Nape Nnauye (Mtama)
na Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), walitaka tathmini ifanyike kabla ya
kuanza kwa mradi huo.
Wamehoji
kitendo cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutangaza tenda
ya kukata miti katika pori hilo, tenda inayohusisha ukataji miti zaidi
ya mita za ujazo 3,495 na kwamba idadi ya miti inayokatwa ni sawa na
ukubwa wa Mkoa wa Dar es Salaam huku ikijulikana wazi kuwa tathmini
bado haijakamilika.
Katika
maelezo yake ya leo, Makamba amesema tathmini inafanyika ili kujua
athari na namna ya kukabiliana nazo, “lazima sheria ifuatwe ikiwamo
kufanya tathmini ya athari ya mazingira, ndicho kinachofanyika hivi sasa
kuhusu mradi huo.”
“Tanesco
walikuja NEMC (Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira)
kusajili mradi wa Stigle’s Gorge ili kufanya tathmini ya mazingira.
Baada ya kuandikisha Tanesco walimchagua mshauri ambaye ni Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam kwa sababu ni kazi ya kisayansi.”
Makamba
amesema tayari shirika hilo limeshapeleka ripoti katika ofisi yake
baada ya kufanya tathmini hiyo na kinachofuata ni NEMC kutuma timu kwa
ajili ya kujiridhisha kuhusu yaliyoandikwa katika mradi na yanayoonekana
kama ni kweli.
Amesema
baada ya hapo kamati ya ufundi ya ushauri itazungumza na wadau wote
katika eneo la mradi na kuthibitisha taarifa zilizopo kuhusu mradi
husika.
No comments