Breaking News

Ujenzi bwawa la umeme mto Rufiji kuanza Julai

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema kuwa hadi kufikia Julai mwaka huu, ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme katika mto Rufiji utakuwa umeanza.

Ameyasema hayo  leo Aprili 3, wakati wa hafla ya kuzindua kituo cha kufua umeme Kinyerezi awamu ya pili.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo ni Rais John Magufuli.

Dk Kalemani amesema mradi huo wa miaka mitatu utakamilika kwa wakati.

Amesema hatua inayoendelea sasa ni kutafuta mkandarasi ambaye hadi kufikia Julai atakuwa ameshapatikana kwa ajili ya kuanza kazi.

“Sasa tunamuandalia mazingira ili akipatikana aanze kazi bila kikwazo, tumemboreshea barabara na tumeshapeleka umeme,” amesema Dk Kalemani.

Akizungumzia suala la umeme wa uhakika, Dk Kalemani amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu watakuwa wamekamilisha uimarishaji wa miundombinu.

“Umeme upo mwingi wa kutosha na wa ziada, kinachofanyika sasa ni kuboresha miundombinu hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu tutakuwa tumelikamilisha hilo na umeme kupatikana wakati wote na katika majira yoyote,” amesema Dk Kalemani.

No comments