Breaking News

TPA yatoa msaada Wodi ya watoto Muhimbili


MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) jana ilitoa msaada wenye thamani ya Sh. milioni 10, ikiwamo viti vinavyotumika kubebea mgonjwa na kifaa cha kupima joto, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akikabidhi msaada huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Nuru Mhando alisema utakwenda kutatua changamoto ambazo zilikuwa zinakabili jengo la Wodi ya Watoto katika hospitali hiyo.

Mhando alisema TPA inatambua na kuthamini dhamira na kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kufikisha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wote.

"Ni wajibu wetu kushiriki katika huduma za kijamii  kwani wao ndiyo wanatuletea faida na kufanya  tuendelee kufanya biashara, na ndio maana tumeamua kutoa msaada huu," alisema Mhando.

Aidha, Mhando alisema TPA imekuwa ikitenga faida yake kwa kila mwaka wa fedha kwa matumizi ya misaada ya kuboresha jamii, hasa katika sekta za elimu, afya, maendeleo kwa jamii na kunusuru waliopatwa na majanga pamoja na maafa.

Alisema katika kuadhimisha miaka 13 tangu TPA kuanzishwa wameamua wiki hii kusherehekea kwa kutoa  mchango huo wa viti vya magurudumu 20 na vipima joto 40 ili kusaidia Wodi ya Watoto.

"Tunaamini msaada huu utasaidia kuhudumia watoto kwa wakati mmoja na kutatua changamoto ya ukosefu wa vifaa hivi mlilokuwa mnakabiliana nalo," alisema Mhando.

Mkurugenzi huduma za uuguzi wa MNH, Agnes Mtawa aliishukuru TPA kwa msaada huo na kwamba utasaidia katika kuimarisha huduma wanazozitoa kwani walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya vifaa hivyo.

Alisema katika wodi hiyo kuna watoto zaidi ya 300 ambao wamelazwa na viti vya kubebea wagonjwa ambavyo wamepatiwa vitasaidia kumbeba mtoto na kumpeleka kwenye huduma za vipimo.

TPA imefanikiwa kukusanya Sh. bilioni 420 kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai mwaka jana baada ya kuongezeka kwa shehena bandarini.

Kiasi hicho ni ongezeko la Sh. bilioni 60 sawa na bilioni 10 kila mwezi kwa wastani ukilinganisha na kipindi hicho hicho mwaka 2016 ambapo TPA ilikusanya Sh. bilioni 360.

Aidha, kwa mwaka huu wastani wa makusanyo umepanda tena kwa kufanikiwa kukusanya Sh. bilioni 72.3 kwa kipindi cha Januari pekee huku Februari ikikusanya Sh. bilioni 74.89.

No comments