Breaking News

SERIKALI YATOA BILIONI 2.6 MWANZA


Serikali imepeleka shilingi bilioni 2.6 katika Jiji la Mwanza kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa vituo vya afya ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Hayo yalibainika wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokagua na kuweka jiwe la msingi la kituo cha afya cha Karume kilichopo kwenye kata ya Bugogwa wilayani Ilemela akiwa katika siku ya sita ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Waziri Mkuu amesema uboreshaji huo ulihusisha ujenzi wa chumba cha upasuaji, maabara, chumba cha kujifungulia, jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na wanaume.

"Nimeridhishwa na uboreshaji wa kituo hichi, serikali inatarajia kuletaa shilingi Milioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali. Lengo la serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi, uboreshaji wa kituo cha afya cha Karume umegharimu takriban shilingi milioni 497 hadi hivi sasa", amesema Majaliwa.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema "mkakati wa Rais Dkt. John Magufuli ni kuimarisha sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu karibu na maeneo yao ya makazi".

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile amesema serikali imetoa shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya afya jijini Mwanza.

Dkt. Faustine amesema fedha hizo zinalenga kuboresha vituo hivyo ili kuviwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi wa jiji zikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, upasuaji na maabara.

No comments