Breaking News

MAHAKAMA YAMFUTIA KESI UHURU KENYATTA


Mahakama Kuu Jumanne iliamua kwamba mashtaka ya uhalifu au madai hayawezi kufunguliwa dhidi ya Rais juu ya utendaji wake wa kazi katika kipindi ambacho alikuwa madarakani.

Kutokana na msingi huo wa kisheria Jaji Chacha Mwita aliliondoa jina la Rais Uhuru Kenyatta kutoka kwenye kesi iliyofunguliwa na mwanaharakati Okiya Omtatah akipinga uamuzi wake wa kuteua makatibu wakuu na makatibu tawala.

Ingawa Jaji Mwita hakutoa sababu za kuliondoa jina la Rais Kenyatta kutoka kwenye kesi, kwa namna fulani ni kama alikubaliana na maoni ya Mwanasheria Mkuu kwamba Rais ana kinga ya kutoshtakiwa.

"Kwa maoni yangu, jina la Rais halipaswi kuwemo katika ombi hili. Nitaeleza sababu katika hukumu ya mwisho," alisema kwa ufupi.

Mwanasheria mkuu kupitia mwanasheria mwandamizi Jennifer Gitiri, aliomba mashtaka hayo yafutwe na kuondolewa kwa jina la Rais Kenyatta katika suala linalojadiliwa kwamba ni kinyume cha katiba kuanzisha mashtaka yoyote dhidi ya Mkuu wa Serikali.

"Tunasisitiza kwamba rais hawezi kushtakiwa kwani anafurahia kinga ya rais," aliongeza.

Gitiri alimwambia Jaji Chacha kuwa hakuna ulazima kwa Rais Kenyatta kuingizwa katika suala hili kwa kuwa AG ana uwezo wa kuiwakilisha serikali ya kitaifa katika madai yoyote.

"Maombi hayatapata pigo lolote ikiwa jina la Rais Kenyatta litaondolewa katika kesi hii," aliongeza.

Bunge kupitia kwa mwanasheria Mbarak Awadh Ahmed alijihusisha na mjibu maombi mwanasheria mkuu kwamba amewasilisha maombi ya kutafuta kupinga mamlaka ya mahakama kusikiliza kesi iliyofunguliwa na Omtatah.

Kikundi cha vijana, kilichodai kina maslahi katika kesi hiyo kilimwambia Jaji Mwita kuwa chini ya sheria ya kimataifa, rais aliyeko madarakani, wakuu wa serikali na mabalozi wana kinga ya kutoshtakiwa.

Katika kesi hiyo, Omtatah aliwashtaki Rais Kenyatta, Tume ya Utumishi wa Umma, Mwanasheria Mkuu na Spika wa Bunge juu ya uteuzi wa Baraza la Mawaziri.

No comments