UKAWA WATISHIA KUSUSIA UCHAGUZI JIMBO LA NYALANDU.
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa endapo Tume ya Uchaguzi na Serikali haitasogeza mbele uchaguzi mdogo wa Wabunge unaotarajiwa kufanyika Januari 13, 2018 basi UKAWA hawatashiriki uchaguzi huo.
Mbowe amesema hayo jana wakati akiongea na waandishi wa habari kwa niaba ya UKAWA kuwa serikali pamoja na Tume ya Uchaguzi inapaswa kuahirisha uchaguzi huo kwanza ili ifanyike tathmini na wadau wa siasa waweze kuzungumza mambo mbalimbali ambayo wamejifunza kupitia uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika hivi karibuni kwani kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria, taratibu na haki za binadamu.
"Miaka miwili ya Rais Magufuli imetupa funzo kubwa sana kwamba mambo siyo sawasawa na sisi kukimbilia kwenda moja kwa moja kwenye uchaguzi katika mazingira haya tunaona kwamba tunaliingiza Taifa katika mpasuko mkubwa sana.
"Sisi kama vyama vya upinzani tunaamini kabisa kuendelea na uchaguzi huu tutakuwa hatulitendei haki taifa, sisi tunaamini katika hatua ya sasa uchaguzi huu unastahili kuaihirishwa, hivyo ni rai yetu kwa serikali na msimamizi wa uchaguzi kuona umuhimu wa kuarisha kwanza uchaguzi huu" alisema Mbowe
Aidha Mbowe aliendelea kusema kuwa endapo Serikali na Tume ya Uchaguzi haitaiona umuhimu wa kuahirisha uchaguzi huo basi wao kama UKAWA hawatashiriki katika uchaguzi huo wa Januari 13, 2017.
"Kuendelea kushiriki chaguzi za kuumiza watu, kufunga watu, chaguzi za kuvunja amani hazitujengi kama taifa bali tunaongeza mpasuko na ufa kati yetu, hivyo sisi rai yetu uchaguzi huu usogezwe mbele wadau tukae kwanza, vyama vya siasa tuzungumze hivi kweli tumechagua uchaguzi ukawe wa mapanga, visu na marungu, hivi kweli tumeshakubaliana mawakala watolewe vituoni?
"Tukishakubaliana kuhusu haya na kwanini yalikiukwa ndiyo uchaguzi ufanyike. Kama Tume ya Uchaguzi na Serikali itapuuza sisi UKAWA hatutakuwa tayari kushiriki uchaguzi wa Januari 13, 2018" alisema Mbowe
No comments