“TIMU YA TAIFA SI SEHEMU YA KUJIFUNZIA UKOCHA”-MWAMBUSI ARUSHA DONGO
Kocha aliyetamba na kikosi cha Mbeya City Juma Mwambusi ametoa maoni yake kuhusiana na timu ya taifa ya Tanzania bara ‘Kilimanjaro Stars’ kufanya vibaya kwenye mashindano ya Chalenji 2017 ambapo amesema, timu ya taifa sio mahali pa kujifunzia ukocha.
Mwambusi ambaye amewahi kufanya kazi kama kocha msaidizi kwenye timu ya Yanga ameonesha kusikitishwa na matokeo mabovu ya Kili Stars kwenye mashindano ya mwaka huu na kuongeza huenda ugeni wa mwalimu ukawa moja ya tatizo kwa timu hiyo kushindwa kufanya vyema.
“Kinachosikitisha watanzania ni timu yetu kufanya vibaya sana katika mashindano ya Chalenji yanayoendelea kule Kenya. Kubwa kama mwalimu ni kuelezana ukweli, watanzania wanataka matokeo mazuri kitu ambacho kocha aliyeteuliwa na wachezaji lazima wajitume na kujitolea kwa ajili ya nchi yao.”
“Timu ya Taifa watu wanaitegemea ni kigezo gani TFF wanakitumia kuteua kocha ni swali ambalo nimekuwa nikiulizwa na wadau wengi wa soka kwa sababu wanaamini kutokana na taaluma yangu na uzoefu huenda nikawa najua, lakini hata mimi sifahamu TFF ndio wenye majibu na wanatakiwa kuwajibu watanzania wapenda michezo kwamba ni vigezo vipi wanavyovitumia.”
“Mwalimu huyu ni mgeni katika soka la Tanzania labda kama alicheza lakini hajafundisha kwa sababu lazima ufundishe vilabu vya ligi kuu ili uweze kuteuliwa mwalimu wa timu ya taifa, lakini sio kufundisha tu umefanya nini katika klabu au vilabu ulivyofundisha. Una wasifu mzuri unawajua watanzania unajua utamaduni wa wachezaji wetu, kwa sababu mwalimu anaweza kuwa mzuri lakini anafundisha katika mazingira yapi na yeye katoka mazingira gani?”
“Watanzania wataendelea kuumia hadi lini kutokana na matokeo ya timu yao ya taifa? Isiwe sehemu ya kujaribia makocha ni kutowapa thamani watanzania ambao mioyo yao inapenda sana matokeo mazuri kutoka kwa timu yetu.”
“Nakumbuka Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassani Mwinyi aliwahi kusema “timu yetu imekuwa kichwa cha mwendawazimu” kwa hiyo kuifuta hii kauli ni lazima tufanye vizuri. Inatakiwa timu iwe na mwelekeo, naishauri TFF kwamba walimu wapo waliofundisha ligi kuu wamefanya vizuri wanatakiwa wapewe nafasi wafundishe timu ya taifa tumechoka kuumia, timu ya taifa sio sehemu ya kwenda kujifunzia au kujaribia.”
“Wachezaji tutawalaumu lakini labda waliletewa utamaduni ambao hawajauzoea na wao wanatakiwa kujituma katika timu yao kwa sababu sisi watanzania tunaumia.”
No comments