Breaking News

KIKOSI CHA BILIONI MOJA CHA SIMBA


BAADA ya Jumapili iliyopita mfanyabiashara bilionea na mwanachama wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ kushinda tenda ya kuwa mwekezaji mkubwa ndani ya Klabu ya Simba, alitangaza mikakati mbalimbali atakayoifanya ili kuibadilisha sura ya klabu hiyo.

Miongoni mwa mambo aliyoyabainisha ni kwamba, atahakikisha ndani ya mwaka mmoja anaibadilisha timu hiyo ili iweze kupambana na timu kubwa Afrika kama TP Mazembe ya DR Congo na Zamalek ya Misri.

Katika kuibadilisha Simba ili iweze kupambana na timu kubwa barani Afrika, Mo alisema kila msimu atatenga kiasi cha Sh bilioni moja kwa ajili ya usajili, fedha ambazo zimeonekana kuwa nyingi katika kujenga kikosi bora na cha ushindani.

Fedha hizo zina uwezo wa kumnunua mchezaji yeyote ndani ya Afrika bila ya kizuizi chochote, kilichobaki ni benchi la ufundi kusema inamtaka mchezaji gani, basi fedha za Mo zitatumika kumsajili.

Wachezaji matata kwa sasa ndani ya nchi hii kama Pappy Kabamba Tshishimbi, Ibrahim Ajibu, Obrey Chirwa na Kelvin Yondani ambao wote wanaichezea Yanga, kama wakitakiwa na Simba, basi wanaweza kusajiliwa kwa fedha hizo na chenji ikabaki.

Mbali na hao, Simba inaweza kwenda nje ya Tanzania kuchukua majembe mengine kadhaa yanayoweza kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho kikawa bora zaidi na kupambana na timu tishio Afrika. Miongoni mwa nyota hao ambao wanaweza kusajiliwa na Simba ambao kwa sasa wapo kwenye kiwango bora na wanaweza kuimarisha zaidi kikosi hicho, ni kiungo wa kati Salif Coulibaly anayeichezea TP Mazembe na beki, Richard Kissi Boateng kutoka SuperSport ya Afrika Kusini.

Nyota hao kwa pamoja wanaweza kugharimu si chini ya Sh milioni 500, katika usajili wao kutokana na viwango vyao na timu wanazotoka ukizingatia kwamba wapo kwenye vikosi vya kwanza. Ukiachana na hao, kwa wastani, Yondani thamani yake ni Sh milioni 60, Ajibu (Sh milioni 50), Tshishimbi (Sh milioni 100) na Obrey Chirwa (Sh milioni 200) pamoja na Ngoma ambaye hivi karibuni mkataba aliouongeza unatajwa kuwa na thamani ya Sh milioni 90 ambazo jumla unapata Sh milioni 500.

Baada ya wachezaji wote wakisajiliwa, kikosi hicho kinaweza kuwa hivi, Aishi Manula, Richard Kissi Boateng, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Salim Mbonde, Kelvin Yondani, James Kotei, Shiza Kichuya, Salif Coulibaly, Emmanuel Okwi, Obrey Chirwa na Haruna Niyonzima.

Wakati hao wakianza, huku benchi kuna, Erasto Nyoni, Mzamiru Yasin, Ajibu na Tshishimbi hakika fedha hizo zinaweza kumshawishi mchezaji yeyote akajiunga na timu hiyo.

No comments