Breaking News

ZITTO KABWE KUFUNGUA KESI MAHAKAMANI

Kiongozi wa ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Mh. Zitto Kabwe amesema watafungua kesi mahakamani kupinga baadhi ya vifungu vilivyomo katika Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 ambayo amedai inanyima uhuru wa wananchi kuchambua takwimu

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya kitengo cha upelelezi wa makosa ya kifedha kilichopo Kamata, Kariakoo jijini Dar es Salaam, Zitto amesema haiwezekani kukawa na mamlaka moja ya kutoa takwimu.

"Tunataka kufungua kesi mahakamani kupinga sheria ya takwimu kuzuia watu kuchambua, huko ndiko ukweli utajulikana na wananchi watajua sheria hii ilivyo. Hii itakuwa kesi ya kwanza kwa sheria hii kupelekwa mahakamani," amesema Zitto.

Amesema, "Tuna taarifa ambazo hatukuzitoa, tukifika mahakamani tutazitoa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu haiwezi kusema una hatia au la kwa kuwa wao si Mahakama. Tungefurahi kama jambo hili lingekwenda mahakamani" Zitto

Ameongeza kwamba "Sisi tulitumia takwimu zao kuchambua na tumewaeleza polisi kwamba tutawaeleza zaidi tukifika mahakamani."

Kuhusu tuhuma za uchochezi zinazomkabili Mh. Zitto amesema kwamba , “Nimeripoti leo kama nilivyotakiwa lakini nimeelezwa nirudi tena Ijumaa Novemba 17, 2017 wanadai wanasubiri chaji kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtakana baada ya hapo wataona kama watanipeleka mahakamani au la.''

Hata hivyo Kiongozi huyo ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini amesema kwamba kesho atarudi tena kituoni hapo tena kesho muda wa asubuhi kwakuwa anatuhumiwa kwa kesi mbili ya sheria ya takwimu na makosa ya mitandao.

No comments