Breaking News

Mkurugenzi Mkuu Wa Kampuni ya Acacia AJIUZULU

Wakati utekelezaji wa makubalino baina ya Serikali na Barrick ukisubiriwa, Ofisa Mtendaji Mkuu na Ofisa Mkuu wa Fedha wa Kampuni ya Acacia, wametangaza kujiuzulu kuanzia leo Alhamisi.

Kwenye barua yake, Ofisa Mtendaji Mkuu, Brad Gordon amesema anataka kurudi nyumbani Australia kusimamia masuala ya familia yake wakati Ofisa Mkuu wa Fedha, Andrew Wray akisema amepata fursa nzuri zaidi sehemu nyingine.

“Pamoja na uamuzi huo, wote wataendelea kuhudumu kwenye nafasi hizo wakati wakikabidhi majukumu ya ofisi kwa warithi wao,” imesema taarifa ya Acacia iliyotolewa leo Alhamisi asubuhi.

Kuziba nafasi hizo, Bodi ya Wakurugenzi wa Acacia imemtangaza Peter Geleta kuchukua majukumu ya ofisa mtendaji mkuu baada ya Gordon na Jaco Maritz kusimamia masuala yote ya fedha za kampuni hiyo.

Wote wawili walikuwa watendaji wa Acacia kwa muda mrefu. Geleta alikuwa mkuu wa oganaizesheni wakati Maritz alikuwa meneja mkuu wa idara ya fedha.

“Licha ya majukumu ya uendeshaji, Geleta atahudhuria vikao vya bodi vitakavyofanyika mwishoni mwa mwaka huu badala ya Gordon na kuifanya idadi ya wajumbe kuendele akubaki saba,” imesema taarifa hiyo.

Kwa miezi miwili iliyobaki, makabidhiano ya ofisi yataendelea kufanyika mpaka Januari Mosi, mwakani yatakapohitimishwa na uongozi mpya kuendelea kutekeleza majukumu yake.

Oktoba 19, Serikali na Kampuni ya Barrick Gold Mine inayomiliki asilimia 63.9 ya hisa za Acacia ilitangaza makubaliano yaliyoafikiwa baada ya majadiliano ya takriban miezi mitatu ambapo kampuni hiyo ilikubali kutekeleza masharti yote ya sheria mpya za madini pamoja na kulipa Dola 300 milioni za Marekani wakati majadiliano kuhusu kodi yakiendelea.

Oktoba 20, Wray aliwaambia waandishi wa habari kwamba Acacia haina uwezo wa kulipa kiasi hicho kwa mkupuo.

No comments