Breaking News

KIJUSO WA MBEYA CITY ATAMBA KUIFUNGA SIMBA JUMAPILI

Kikosi cha Simba kinatarajia upinzani mkubwa kwenye pambano la Jumapili wakati watakapoikabili Mbeya City uwanja wa Sokoine Mbeya

Kocha msaidizi wa Mbeya City, Mohamed Kijuso ameitahadharisha klabu ya Simba, kuwa kujiandaa na kipigo katika pambano lao la Jumapili litakalofanyika kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Kijuso ameiambia Goal, wameiona Simba, walipocheza dhidi ya Yanga Jumamosi iliyopita na kubaini mapungufu mengi kwenye kikosi hicho ambacho ameahidi kuyafanyia kazi ili kupata ushindi.

"Msimu uliopita tulipata sare ya mabao 2-2, kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam, safari hii tunataka kuwafunga mbele ya mashabiki wetu kwasababu dhamira tuliyokuwa nayo ni kupanda kwenye nafasi za juu kama ilivyo kwa timu nyingine," amesema Kijuso.

Kocha huyo msaidizi amesema maandalizi yao kwa ajili ya pambano hilo la Jumapili yanakwenda vizuri na kwenye kikosi chao hakuna mchezaji yeyote aliyokuwa majeruhi jambo ambalo linawapa matumaini ya kutimiza ahadi yao kwa mashabiki.

Amesema anatambua kuwa Simba ni timu kubwa na inaundwa na wachezaji wenye majina makubwa lakini hilo haliwatishi watakacho kifanya hakitokuwa na tofauti ya kile walichofanyiwa na Yanga na kujikuta wanacheza kwa kuzuia kwa kuhofia kufungwa.

Mbeya City, ni moja ya timu ambayo imekuwa na rekodi ya kuisumbua Simba, na mara kadhaa Simba wamekuwa wakipoteza mchezo dhidi ya vijana hao wa Gren City ambao kwasasa wanafundishwa na kocha Ramadhani raia wa Burundi baada ya uongozi kumtimua kazi Kinnah Phiri raia wa Malawi.


No comments