Zitto Kabwe Amwaga 'Sumu' Mbagala, Dsm
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amezindua kampeni za chama hicho za uchaguzi mdogo wa udiwani akiahidi iwapo kitachaguliwa kitaondoa hali ngumu ya uchumi na ukiukwaji wa haki.
Zitto akizungumza katika Kata ya Kijichi mkoani Dar es Salaam leo Jumapili Oktoba 29,2017 amesema wananchi watumie uchaguzi mdogo katika kata 43 nchini utakaofanyika Novemba 26,2017 kutuma salamu kwa CCM kwamba hawaridhishwi na jinsi nchi inavyoendeshwa.
Amesema mtu akitaka kujua uchumi unasinyaa, aangalie alikuwa akipata shilingi ngapi na sasa anapata ngapi.
Zitto amewaomba wananchi wa Kijichi kumchagua mgombea udiwani wa ACT Wazalendo, Edgar Mkosamali ili kuwe na mabadiliko kwenye baraza la madiwani la Halmashauri ya Temeke.
Kiongozi huyo amelalamikia kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara akidai ni ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi na pia kuwanyima wananchi haki ya kukusanyika kwenye vyama vyao.
"Leo hii tunasubiri uchaguzi mdogo ndiyo tufanye mikutano ya hadhara. Kama hupendezwi na haya yote, onyesha chuki yako kwa kumchagua Mkosamali," amesema.
Zitto amesema chama hicho kikipewa ridhaa ya kuongoza Kata ya Kijichi kitaifanya kuwa ya mfano katika kutatua kero zinazowakabili wananchi.
"Kwa udogo na uchanga wetu tutawapa utumishi uliotukuka. Tunataka kuifanya Kata ya Kijichi kuwa ya mfano," amesema Zitto.
Akizungumzia uongozi, Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja amewaeleza wananchi kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likiwanyanyasa jambo ambalo ni ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi.
Maganja amesema lazima nchi iongozwe kwa misingi ya Katiba na sheria ili kuleta haki kwa jamii.
Mgombea udiwani katika kata hiyo, Mkosamali amesema anatambua matatizo yaliyopo na amejipanga kuhakikisha anayatatua.
Amesema hatalala bali atazunguka kila mahali kutafuta wafadhili kwa ajili ya kuleta maendeleo kwenye kata hiyo.
No comments