WATU WATANO WAFARIKI KIMARA KWA KUNYWA GONGO
Watu watano wamefariki dunia baada ya kunywa kitu kinachosadikiwa kuwa gongo eneo la Kimara jijini hapa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Daniel Nkungu amesema kwa nyakati tofauti kuanzia jana Jumanne jioni hadi saa nane usiku wa kuamkia leo Jumatano walipokea miili ya watu wanne waliofariki kutokana na kunywa kitu kinachosemekana kuwa ni gongo kutoka Kimara.
“Saa nane usiku aliletwa mwanamume aliyekuwa hai lakini katika hali mbaya na alifariki wakati anaendelea kupata huduma, hivyo kufanya waliokufa kuwa watano,” amesema.
Dk Nkungu amesema kati ya waliokufa mwanamke ni mmoja na miili yao imepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha tukio hilo akisema atatoa ufafanuzi.
Taarifa za awali zilizopatikana eneo la tukio zimesema waliokufa wanasadikiwa kuwa tisa katika eneo la Kimara Stop Over na kwamba wengine kadhaa wamelazwa kwa matibabu Mwananyamala.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Stop Over, Magreth Mugyabuso amesema, “Watu hawa inadaiwa walinunua gongo ya viwandani wakaichanganya na vitu vingine, nadhani katika utengenezaji kuna mambo walikosea hivyo kusababisha madhara hayo,” amesema Mugyabuso.
Amesema alipata taarifa za tukio hilo jana saa sita usiku baada ya kupigiwa simu na polisi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Saranga, Dandus Kijo ameeleza kusikitishwa na vifo vya watu hao. Amewaasa wananchi kuacha kunywa pombe ambazo hazijapimwa ili kuokoa maisha yao.
“Naelekea hospitalini Mwananyamala kuangalia wagonjwa walionusurika kwa kuwa nasikia wengine wamekuwa vipofu,’’ amesema Kijo alipozungumza na gazeti hili saa nane mchana.
No comments