Breaking News

WALIMU WAGEUZA MTI OFISI

WALIMU WA SHULE YA MSINGI BUMERA, WILAYANI ITILIMA, MKOANI SIMIYU WAKIWA WAMEKAA KATIKA GOGO CHINI YA MTI SHULENI HAPO AMBAPO WANADAI WAMEKUWA WAKIPATUMIA KAMA OFISI YA WALIMU KUTOKANA NA KUKOSA OFISI KWA ZAIDI YA MIAKA 10. PEMBENI NI MWANDISHI WA MAKALA HII.

UKIFIKA shule ya Msingi Bumera,  iliyoko zaidi ya  kilomita 30 kutokea Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Mkoani Simiyu,  unaweza kudhani ni shule ya awali kwa jinsi majengo na mazingira ya shule hiyo yalivyo.

Katu si rahisi kwa mtu kufikiria kuwa mazingira ya shule hiyo yanaweza kwenda sawia na ile Methali isemayo ‘uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti.’

Sikupenda kuamini kuwa shule hiyo inaweza kuwa na mazingira ya namna ile ingawa mazingira yake ni mazuri na bora kwa kujifunzia na kufundishia kutokana na mandhari ya kuvutia huku miti mirefu ikiipamba shule hiyo.

Pamoja na mandhari hiyo nzuri kwa kujifunzia na kufundishia bado nikajikuta ninakaribishwa kwenye gogo, tena lililo chini ya mti.

Nilijiuliza kwa nini mwenyeji wangu aliyenipokea alinifikisha chini ya mti na si ofisini, lakini kwa ugeni niliokuwa nao niliamua kunyamaza kwa lengo la kupata nilichokuwa nakihitaji.

Hata hivyo, wakati nilipokuwa nabisha hodi, akilini mwangu niliamini kuwa jengo lile ni moja kati ya nyumba za walimu shuleni hapo, kumbe sikuwa sahihi kabisa kutokana na jibu nililopewa na mwenyeji huyo.

Kwa haraka sikupata jibu mpaka pale nilipoanza kujitambulisha na kuuliza lililomo moyoni mwangu.

Mwenyeji wangu Magesa Lubega ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi Bumera, aliniambia kuwa ile ni shule ya msingi na jengo alilokuwa amenipokelea si nyumba ya mwalimu bali ni jengo la ofisi ya walimu ambalo linatarajiwa kukamilika muda wowote.

Huku akiwa amevalia shati jekundu la mikono mirefu mwalimu huyo alionekana akiwa anafurahia sana ujio wangu na kunipeleka hadi chini ya mti na kisha wote tukaketi pamoja na walimu wenzake.

Wakati tukiwa tumeketi chini ya mti nilimhoji ili nifahamu yeye ni nani na anahusika vipi katika jengo lile ambalo lilikuwa jipya na ujenzi wake ukiwa bado haujamalizika.

“Mimi ni Mwalimu Magesa Lubega nafundisha katika hii shule ya msingi Bumera iliyopo Wilayani Itilima na hapa chini ya mti tulipokaa ndipo kimsingi kwa wakati huu ni ofisi ya walimu …karibu sana ujisikie nyumbani,” anasema mdomoni akiwa na tabasamu na kuongeza:

“Tunafurahi kwa kututembelea na kujionea adha na mateso tunayoyapata katika maeneo yetu ya kufanyia kazi kutokana na mazingira yenyewe kutokuwa rafiki kiasi cha kumvutia na kumshawishi mwalimu awe na ari ya kufundisha.”

Anasema wamekuwa wakifanya shughuli zao za kiutendaji za kuandaa vipindi, mitaala na mambo mengine chini ya mti huo kwa zaidi ya miaka 10 sasa kwa sababu shule hiyo haina ofisi.

KUKOSEKANA VITENDEA KAZI

Mwalimu Lubega anafafanua kuwa wamekuwa wakipata shida katika utendaji wao wa kazi, kwa kuwa muda mwingi huwa wanautumia kukaa kwenye gogo na kufanya kazi zao bila hata kuwa na meza.

“Na badala yake tumegeuza mapaja yetu kuwa ndiyo meza za kutumia, hali ambayo inatunyima muda wa kufanya kazi zetu za ualimu kwa ufanisi na uhakika,”anasema.

Anahabarisha kuwa siku moja walikutwa na Mbunge wa jimbo hilo wakiwa wamekaa nje wanasahihisha madaftari ya wanafunzi.

Mwalimu Lubega anabainisha kuwa hali hiyo ilimkera mbunge huyo na ndipo alipoamua kuwajengea jengo moja kubwa la ofisi ya walimu pamoja na vyumba vinne vya madarasa ili kuwapunguzia adha wanayoipata.

MIUNDOMBINU

Anasimulia kuwa shule hiyo imekuwa na uhaba wa vyumba vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu kutokana na kuwa ya siku nyingi.

Anasema shule hiyo ilijengwa kwenye mwaka 1952, kipindi ambacho hakikukuwa na idadi kubwa ya wanafunzi na walimu.

“Shule hii ilijengwa miaka ya nyuma sana hivyo kwa wakati huo ilikuwa ikikidhi matakwa ya walimu na wanafunzi. Zamani hizo ilikuwa na kiofisi kidogo ambacho kwa sasa hakifai kutumiwa na walimu 11waliopo kwa hivi sasa shuleni hapa,” anasema na kuongeza:
“Kwa sasa chumba hiki tumekifanya ofisi ya mkuu wa shule na stoo ya kuhifadhia nyaraka muhimu za ofisi.”

Hata hivyo, anasema sasa wanatarajia kuondokana na tatizo hilo mara jengo la ofisi linalojengwa kwa msaada wa
mbunge wa jimbo hilo Njalu Silanga litakapomalizika.

Mbunge ambaye pia ameamua kuwajengea na vyumba vinne vya madarasa.

“Tulikuwa tukipata adha ya upepo ,vumbi na kunyweshewa mvua maana hakukuwa na sehemu nyingine ya kujihifadhi mbali na kurundikana kwenye vyumba vya madarasa ambavyo navyo vimejaa wanafunzi,” anasema.
MWALIMU MKUU

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Andreycus Nyaki anasema suala la walimu kukabiliwa na mazingira duni ya kazi kama ya kukosa ofisi na nyumba za walimu kumewafanya waone kama vile hawathaminiwi.

Nyaki anasema kitendo cha wao kufanya kazi katika mazingira ambayo si rafiki kinawatofautisha kimsingi na walimu walio mjini.

“Hatukuwa na ofisi ya walimu kwa zaidi ya miaka 10, lakini hata nyumba za kuishi walimu ziko katika hali mbaya kama zilivyo nyumba nyingi za wanakijiji…ukituuangalia sisi walimu ambao ndio kioo cha jamii huwezi kututofautisha na mwanakijiji au mkulima,” anasema na kuongeza:

“Unaweza ukajiuliza kwa nini ari na morali ya walimu imeshuka? Hapo utakutana na sababu nyingi sana. Ukosefu wa ofisi, mazingira mabovu ya kufundishia, maslahi duni na kukosekana kwa motisha ni mambo ambayo yameendelea kuwakwaza walimu na kuwaondolea morali wa kuipenda kazi yao kwa bidii.”

CHAMA CHA WALIMU

Naye mmoja wa walimu wa shule hiyo Silusi Mtaki anasema mahusiano ya serikali na walimu kupitia chama chao cha walimu nayo si mazuri kiasi kwamba serikali haikisikilizi chombo hicho na badala yake kinadharauriwa.

Anasema matatizo mbalimbali ya walimu likiwamo suala zima la nyumba za kukaa walimu mpaka sasa hayajapatiwa ufumbuzi.

OFISA ELIMU 

Ofisa Elimu wa hiyo Julius Nestory anasema katika baadhi ya maeneo mengi ya wilaya hiyo bado walimu wanachangamoto nyingi ambazo ni pamoja na uduni wa nyumba, changamoto ya ofisi za walimu na vitendea kazi.

“Hata hivyo, serikali inajitahidi kutatua changamoto hizo kwa awamu hivyo nawanasibu walimu wavumilie kwani ipo siku matatizo yao yatapatiwa majibu ya kudumu,” anasema.

Nestory anabainisha kuwa hakuna mtu yeyote anayependa kuishi kwenye mazingira magumu na kwamba hata walimu walioko vijijini bado wana haki ya kupata huduma sawa na wale wanaoishi mijini, hivyo ipo siku matatizo hayo ya walimu yataisha.

ATHARI ZAKE

Ofisa elimu huyo anabainisha kuwa athari za miundombinu duni zinasababisha wakati mwingine walimu waripoti na kuondoka mara wakutapo mazingira hayo yasiyo rafiki na hatimaye kuwa chanzo cha shule nyingi kuwa na walimu wachache sana .

 “Mazingira kama haya hayampi mwalimu ari na motisha wa kufanya kazi…. Pia hayamuwezeshi mwanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yake,” anasema na kuongeza:

“Kimsingi mazingira duni ya utoaji wa elimu huenda yakawa sababu ya baadhi ya wazazi wenye uwezo kifedha kusomesha watoto wao shule binafsi za hapa nchini na hata zilizoko nje ya nchi.”
MBUNGE

Naye mbunge wa jimbo hilo anasema ana wajibu wa kuhakikisha walimu wanaishi katika mazingira mazuri ya kuwawezesha kufanya kazi yao vizuri ya kufundisha pamoja na kuishi.

“Nilisikitishwa niliposhuhudia shule hiyo haina ofisi ya walimu na badala yake wakitumia mti kama ofisi yao, ndipo nilipoamua kuwajengea ofisi pamoja na vyumba vinne vya madarasa ili kuwapunguzia kero,” anasema.

Silanga anasema yeye na serikali ya awamu ya tano wamedhamiria kutatua kero mbalimbali katika sekta ya elimu na anawaomba walimu wa jimbo lake kuwa wavumilivu kwani changamoto wanazokabiliana nazo ni za muda na zitashughulikiwa.

No comments