Wabunge Wahoji Magari Yao Kukaa Nyuma Msafara wa Rais
Baadhi ya wabunge wamehoji ni kwanini magari ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya yanatangulia mbele huku ya kwao yakiwa ya mwisho katika msafara wa rais pindi anapotembelea majimbo yao.
Hoja hiyo imeibuliwa jana na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilal (CCM), wakati akichangia katika semina ya wabunge wa Kamati za Bunge kuhusiana na masuala ya Kidiplomasia na Itifaki.
Naye Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiku (Chadema), alihoji ni kwanini wao huwa nyuma huku magari ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya yakipeperusha bendera hoja iliyoungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso (Chadema) huku Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah (CUF), akiomba apewe ufafanuzi kuhusiana na mambo ya Itifaki.
“Katika ziara hizo gari la Mkuu wa Mkoa huwa linaongoza mbele likiwa na bendera na kufuatiwa na la Mkuu wa Wilaya kisha gari mbunge huwa la mwisho, katika hili tunaomba ufafanuzi ni kwanini gari la Mbunge huwa ni la mwisho katika ziara,” alihoji Hilal.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba (CCM), alipingana na wabunge wenzake kwa kudai kuwa Mkuu wa Mkoa na Wilaya wana mamlaka ya kupeperusha bendera kutokana na kuwa mteule wa Rais ambapo Rais anachaguliwa na watu nchi nzima tofauti na mbunge ambaye anachaguliwa na watu wa jimbo lake tu.
“Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya anamwakilisha Rais aliyechaguliwa nchi nzima sisi ni vijimbo tu lakini pia wilaya yote ipo chini yake hata kama ni majimbo matano lakini ndiyo viongozi pekee wenye kofia mbili ya kwanza ukuu wa serikali wa eneo husika na pili ndiyo wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo yao,” alisema Mgumba.
Akitolea ufafanuzi jambo hilo, Ofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Kitengo cha Uhusiano wa Kimataifa, Ally Masabo alisema kiitifaki Mkuu wa Mkoa ndiye anayetakiwa kuwa mbele kutokana na kuwa mteule wa Rais.
No comments