Breaking News

SIMBA YAZIDI KUNG`ARA

SIMBA wana kila sababu ya kutabasamu baada ya jana kupata ushindi wake wa kwanza ugenini kwa kuichapa Stand United na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku Laudit Mavugo akianza mambo kwa kutupia nyavuni.

 

SIMBA wana kila sababu ya kutabasamu baada ya jana kupata ushindi wake wa kwanza ugenini kwa kuichapa Stand United na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku Laudit Mavugo akianza mambo kwa kutupia nyavuni.

Mavugo, ambaye amekuwa akipewa nafasi ndogo katika kikosi cha Kocha Joseph Omog, jana aliingia Uwanja wa Kambarage, mjini hapa na mguu wa bahati baada ya kuifungia Simba bao lililowapa ushindi wa 2-1.

Ushindi huo uliiwezesha Simba kurejea kileleni ikizipiku Mtibwa Sugar na Azam FC wanazolingana nao pointi 11 kila moja kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba ina mabao 14 katika mechi zake tano walizocheza mpaka sasa, huku wavu wake ukitikiswa mara tatu. Mtibwa inafuata na mabao matano ikiruhusu mawili, wakati Azam ina mabao manne na kufungwa moja tu.

Straika huyo kutoka Burundi, aliyekuwa akicheza mechi yake ya pili msimu huu, alifunga bao hilo sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Emmanuel Okwi aliyeshindwa kuonyesha makeke katika mechi hiyo.

Mavugo alifunga bao hilo baada ya kuwahi mpira mbele ya beki wa Chama la Wana na kufunga kwa utulivu mbele ya kipa Frank Muwonge na kuamsha hoihoi za mashabiki wa Simba ambao, walijaza kwa wingi uwanjani hapo.

Kabla ya Mavugo kuandika lake hilo la kwanza kwa msimu huu, Shiza Kichuya aliipa uongozi Simba kwa bao tamu la dakika ya 17 akimaliza pasi Haruna Niyonzima aliyewahi krosi pasi na beki wa pembeni, Erasto Nyoni.

Kichuya alifunga bao hilo kwa shuti kali nje ya 18 na kumuacha kipa Muwonge akiwa hana la kufanya licha ya kujitahidi kuurukia mpira huo uliokuwa na kasi ya 4G.

Chama la Wana ambao mechi iliyopita walipata ushindi wao wa kwanza dhidi ya Mbeya City, ilipata bao la kufutia machozi lililowekwa kimiani na Mzimbabwe Mutasa Munashe, aliyewahi mpira wake wa penalti uliokolewa na kipa Aishi Manula katika dakika ya 52. Hilo lilikuwa bao la sita katika Ligi Kuu Bara kufungwa na mchezaji kutoka Zimbabwe. Licha ya mwamuzi Seleman Kinugani kutoka Morogoro kuamuru adhabu hiyo baada ya beki Ally Shomari kuonekana kama kaunawa mpira, japo picha za marudio zilionyesha kama mpira huo ulimpiga mbavuni wakati akiwania mpira na Adam Salamba. Matokeo hayo yameifanya Simba kuwa na uhakika kukaa kileleni kwa wiki mbili kabla ya Ligi Kuu Bara haijarejea tena baada ya mapumziko mafupi, huku pia nyota wao, Okwi akiendelea kuiongoza orodha ya wafungaji.

Mwanjali alia

Nahodha wa Simba, Method Mwanjali aliwapongeza wachezaji wenzake na hasa Manula kwa kazi kubwa aliyofanya katika mchezo huo, lakini akimlalamikia mwamuzi kwa kuruhusu adhabu ya penalti bila kuwepo kwa kosa lolote.

“Sitaki kuingilia mambo ya waamuzi, ila ukweli hakuona kilichotokea, beki wangu hakuunawa mpira, lakini tunashukuru Manula kafanya kazi ya ziada.” alisema.

Simba: Manula, Shomary, Nyoni, Mbonde, Mwanjali, Kotei, Niyonzima/ Mkude, Mzamiru/Ndemla, Bocco, Okwi/Mavugo, Kichuya.

No comments