Breaking News

Rais Magufuli ampiga dongo Zitto Kabwe kuhusu mapato

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameshangazwa na baadhi ya wanasiasa kuibuka na kusema kuwa, makusanyo ya serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameshuka na hivyo serikali haiweze kutekeleza baadhi ya majukumu yake ya msingi.

Amehoji kwanini vyombo vya ulinzi na usalama haviwakamati viongozi hawa na kuwafikisha mahakamani ili wakathibitishe taarifa hizo kwani wamekuwa wakipotosha umma.

Rais Magufuli ameyasema leo alipokuwa akikabidhi vyeti vya shukrani kwa wajumbe wa kamati mbalimbali  zilizohusika katika mchakato mzima wa madini Ikulu Dar es Salaam, ikiwa ni njia ya kutambua mchango wao mkubwa na wa kizalendo wa kupigani rasilimali za nchi.

Akikanusha taarifa hizo, Rais Magufuli amesema kuwa, ingekuwa ni kweli serikali imeshindwa kukusanya mapato isingeweza kutoa elimu bure kwa wanafunzi, isingeweza kujenga reli kwa kiwango cha kisasa yenye urefu wa kilomita 700 pamoja na kununua meli katika Ziwa Victoria ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu MV Bukoba ilipopata ajali.

Aidha alisema kwamba, mapato ya serikali yangu yamepungua kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa, isingeweza kutekeleza mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji, Strigler’s Gorge ambao hadi sasa Kampuni zaidi ya 75 zimewasilisha maombi zikiomba zabuni ya kutekeleza mradi huo.

Kuna wengine wanasema kuwa mapato ya serikali yameporomoka, kama ni kweli mapato yameporomoka serikali ingeweza kununua ndege sita mpya? Au wanadhani kuwa tumebadilisha hizo ndege na migebuka ya Kigoma? alihoji Rais Magufuli.

Licha ya kuwa Rais Magufuli hakusema moja kwa moja alikuwa akimlenga nani, lakini ushahidi wa kimazingira unaonyesha kuwa alimlenga Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kutokana na kudai kuwa mapato ya serikali yamepungua.

Oktoba 7 mwaka huu kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto Kabwe ambaye nui Mbunge wa Kigoma Mjini aliandika maoni yake akihoji kwanini mapato ya serikali yameshuka. Andiko la Zitto linasomeka, “Mapato ya Serikali Kwa miezi ya Julai na Agosti yameshuka mpaka chini ya Shilingi 600 bilioni. Ni mporomoko mkubwa Sana na sio jambo la kushangilia hata kidogo. Madhara ya kushuka Kwa mapato ni makubwa kwani Mishahara ya Watumishi wa Umma peke yake ni Shilingi 570 bilioni Kwa Mwezi. Kwanini mapato yanashuka?”
Unaweza kusoma andiko la Zitto hapa chini;

Hata leo baada ya Rais kusema kuwa mapato ya serikali hayajashuka na kwamba yapo vizuri ndio sababu wameweza kufanya mambo mengi ikiwamo kulipa gharama za kununua ndege, Zitto Kabwe amejibu kwa kuandika kwamba, serikali imekopa fedha kutoa Uswiss na kwamba sehemu ya fedha hizo ndizo zimetumika kulipia ndege zilizonunuliwa.

“Serikali ya CCM ya awamu ya Tano imekopa $500m kutoka Benki ya CreditSuisse ya Uswiss Kwa riba kubwa Sana. Sehemu ya Fedha hizo zimetumika kulipia Ndege ambazo Serikali inanunua. Wavuvi wa Migebuka Kigoma watahusika kulipa deni Hilo kupitia kodi zao.”

Rais Magufuli ametoa vyeti kwa wajumbe 25 wa kamati za madini akiwemo pia Spika wa Bunge kwa mchango wao na kuweka maisha yao hatarini katika kupigania maslahi ya taifa.

No comments