Breaking News

NEC: Waliopoteza vitambulisho ruksa kupiga kura uchaguzi mdogo wa madiwani

Wapiga kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata 43 unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu.

Hayo yamesemwa jana Jumatatu Oktoba 16, 2017 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima mjini Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi yanayoratibiwa na kuendeshwa na NEC.

Kailima alisema wapiga kura hao wataruhusiwa kutumia vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), hati ya kusafiria na leseni ya udereva.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu namba 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambacho kinasema mpiga kura aliyeandikishwa kwenye daftari atakwenda mwenyewe kwenye kata aliyojiandikisha, kwenye kituo alichopangiwa, kumridhisha msimamizi wa kituo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwamba yeye ndiye mpiga kura kwa kumuonyesha kadi ya kupigia kura lakini kinasema kwamba Tume inaweza ikaelekeza utambulisho mwingine wowote utakaomsaidia mpiga kura kuweza kupiga kura iwapo kadi hana,” alisema Kailima.

Mkurugenzi huyo wa uchaguzi alisema, “Tume kwa kuzingatia kifungu hicho, kuanzia uchaguzi huu imetoa maelekezo kwenye mafunzo haya kwamba Tume imekubali vitambulisho vifuatavyo vitumike, moja ni pasi ya kusafiria, pili ni kitambulisho cha Taifa kilichotolewa na Nida na mwisho ni leseni ya udereva.”

Alisema ruhusa hiyo imetolewa kwa sharti kwamba, “Majina na herufi yaliyopo kwenye kitambulisho hicho yafanane na majina na herufi zilizopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.”

Kailima amesema NEC itakutana na vyama vya siasa hivi karibuni kuwajulisha juu ya maagizo hayo, lakini akasisitiza kwamba tofauti yoyote itakayokuwepo kwenye majina itamnyima mpiga kura fursa ya kupiga kura.

Alisema uamuzi huo umefikiwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo kwa mara ya mwisho liliboreshwa mwaka 2015.

No comments