Breaking News

Jafo aagiza kila mkuu wa mkoa kujenga viwanda vipya 100

Kila mkuu wa mkoa nchini ameagizwa kujenga viwanda vipya 100 katika kipindi cha mwaka mmoja kinachoanzia Desemba 2017.

Akizungumza na wakuu wa mikoa wapya walioapishwa juzi Ikulu jijini Dar es Salaam, waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo aliwataka kuitekeleza ipasavyo sera ya ujenzi wa viwanda.

Jafo alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 2018 kila mkoa uwe umejenga viwanda vidogo na vya kati visivyopungua 100.

Alisema mikoa 26 ya Tanzania Bara inatakiwa kuwa na viwanda vipya vidogo na vya kati visivyopungua 2,600 ifikapo Desemba 2018. Alisema Serikali imekusudia kufikia nchi ya uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda huku akiwataka wakuu hao kuibua viwanda vidogo na vya kati kwa kuhamasisha ushiriki wa viongozi ndani ya mikoa na wananchi katika maeneo yao ya utawala.

Jafo aliongeza kuwa, katika kusimamia utekelezaji wa agizo hilo ofisi yake itaweka utaratibu maalumu wa kupima utendaji kazi wa kila kiongozi wa mkoa kwa kuangalia ushiriki wake wa kuwajengea hamasa viongozi wa chini wakiwamo wakuu wa wilaya na wananchi.

Alisema katika kufanikisha dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, Serikali inaendelea kuweka mkazo na kipaumbele katika upatikanaji wa malighafi za kilimo na kuwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa maofisa ugani wanatekeleza vyema majukumu yao ya kazi. 

Pia, aliwataka wakuu hao wa mikoa kusimamia makusanyo ya fedha za ndani katika halmashauri na kutumia vyema asilimia tano zinazotengwa kuwawezesha wananchi kupata mikopo ili washiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema ili kufanikisha dhana ya uchumi wa viwanda, Serikali haina budi kuwapa msukumo na ushirikiano wa karibu wanasayansi utakaowezesha kuibua viwanda vingi zaidi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kilimo nchini.

Mbali na Malima, wakuu wengine wa mikoa waliohudhuria mkutano huo ni Robert Luhumbi (Geita), Joachim Wangabo (Rukwa), Galesius Byakanwa (Mtwara) na Christine Mndeme (Ruvuma).

No comments