Babu wa miaka 70 jela miaka 30 kwa kubaka mjukuu
Mshtakiwa aliomba Mahakama imwachie huru kwa kuwa ni mzee, hivyo anaweza kufia gerezani.
Chunya. Mahakama ya Wilaya ya Chunya imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Steven Petro (70) mkazi wa Kijiji cha Godima baada ya kumtia hatiani kwa kumbaka mjukuu wake mwenye miaka 12.
Katika utetezi mahakamani, mshtakiwa alikiri shtaka lililomsababishia mtoto huyo maumivu makali na kutokwa damu nyingi.
Hakimu Mkazi, Desdery Magezi akitoa hukumu jana Jumatano alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa hivyo kumtia hatiani mshtakiwa na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela.
Kabla ya hukumu kusomwa, mwendesha mashtaka wa Polisi, Fredrick Philimon alidaia mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 14 nyumbani kwake katika Kijiji cha Godima wilayani Chunya.
Ilidaiwa mshtakiwa alitumia mbinu ya kumtuma mtoto huyo kuchota maji akimpatia Sh500.
Alidai mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Godima na hakufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kutokana na athari alizozipata baada ya kufanyiwa kitendo hicho.
Akitoa ushahidi mahakamani, mtoto huyo alidai haikuwa mara ya kwanza kwa mshtakiwa kumbaka na alikuwa akimtishia kumuua endapo angetoa siri kwa ndugu au kwa uongozi wa kijiji.
Mtoto huyo aliiomba Mahakama kutenda haki na kuchukua hatua kali dhidi ya mshtakiwa kutokana na kitendo cha kikatili alichomtendea na kusababisha ashindwe kufanya mtihani uliofanyika Septemba 6 na 7.
Daktari katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya, Moris Mdoe aliyekuwa shahidi wa pili katika kesi hiyo, aliithibitishia Mahakama kuwa mtoto huyo alibakwa na alikuwa na viashiria vya tendo hilo sehemu zake za siri zikiwemo mbegu za kiume na michubuko.
Alisema uchunguzi ulionyesha mtoto huyo aliingiliwa kwa nguvu kitendo kilichosababisha atokwe damu nyingi.
Mshtakiwa alikiri mbele ya Mahakama kutenda kosa hilo na aliomba imwachie huru kwa kuwa ni mzee, hivyo anaweza kufia gerezani.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Hebel Kihaka aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaojihusisha na matukio ya ubakaji ukiwemo wa watoto wenye umri mdogo.
Hakimu akitoa hukumu alisema utetezi wa mshtakiwa hauna msingi kwa kuwa alifanya hivyo akitambua fika ni kinyume cha sheria na haki za watoto.
No comments