Breaking News

WANANCHI WAVAMIA KIWANDA NA KUVUNJA GETI WAKITAKA AJIRA

Zaidi ya watu 5,000 toka katika maeneo mbalimbali mkoani Morogoro wamevamia na kufanya vurugu katika kiwanda kipya cha kutengeneza mafuta ya kula cha Abood Seed Industries Ltd (Moproco) wakishinikiza kupewa ajira kiwandani humo ikiwa ni siku mbili tu tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzindua kiwanda  hicho.

Maelfu ya wananchi hao waliokutwa na  Mwananchi leo Jumatatu katika eneo hilo walisema wamefika hapo kutafuta ajira baada ya kusikia kuwa Waziri Mkuu ameshakizindua na kutangaza kuwa kitatoa ajira kwa vijana.

Vurugu hizo zilisababisha kuvunjika kwa sehemu ya geti kuu la kuingilia kiwandani hapo hali iliyosababisha askari wa kutuliza ghasia kwenda ili kurejesha hali ya utulivu.

Nasma Rashid ni mmoja kati ya wananchi waliofika kiwandani hapo kutafuta ajira amesema aliamua kufika baada ya kuona kwenye vyombo vya habari kuwa waziri mkuu ameshazindua kiwanda hicho.

“Nilileta barua ya kuomba ajira hapa tangu mwezi Machi mwaka huu hivyo nilivyoona kimeshazinduliwa ndo nikaamua nije ili nijaribu bahati yangu,” alisema Rashid

Paschal Bruno, Mkazi wa Chamwino mjini Morogoro alisema siku ambayo Waziri Mkuu alifika kiwandani hapo alipewa kibarua cha kufyeka nyasi ili kusafisha maeneo ya kiwanda na kulipwa Sh 10,000 hivyo alijua kibarua hicho ni endelevu.

Kwa upande wake Neema Juma mkazi wa mji mpya Morogoro alisema yeye pia alifika siku ya Septemba 2 wakati Waziri Mkuu alipotembelea kiwanda hicho ambapo alipewa kazi ya kufanya usafi kiwandani na kulipwa Sh 6,000.

Mwananchi ilishuhudia viongozi wa kiwanda hicho wakiwa katika lango kuu la kuingilia kiwandani hapo wakiwa na hamaki kutokana na hali iliyojitokeza.

Meneja wa kiwanda hicho,Wilson Ndimgwango alisema wanatarajia kutoa ajira kwa wananchi 150 na ajira hizo zitatolewa kwa awamu kulingana uhitaji wa kiwanda.

“Tumefika hapa asubuhi tukakuta tayari wananchi hawa wameshafika na kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo walivyokuwa wanaongezeka baada ya muda mlinzi akapiga simu kuomba msaada kwani walikuwa wanashinikiza kuingia, ndipo tulipoomba msaada wa polisi,” alisema meneja huyo.

Meneja huyo alisema pamoja na kutoa matangazo mara kadhaa kuwataka wananchi hao kuacha barua zao za maombi ya kazi getini lakini bado wameendelea kuwepo getini.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Ulrich Matei alisema vurugu hizo zilizosababishwa na wananchi waliokuwa wakitaka ajira na ametuma askari kuwepo katika eneo hilo.

“Ni fujo kidogo tu zimetokea na hakuna mtu aliyekamatwa kwani wale ni watanzania na wana haki ya kutafuta ajira, mimi nilipopigiwa simu nilituma vijana wangu wa pikipiki waende wakaangalie hali ikoje,” alisema Kamanda.

Kwa upande wake Mbunge wa Morogoro Mjini ambaye ndiye mmiliki wa kiwanda hicho,Aziz Abood alisema anasikitishwa na hali iliyojitokeza kiwandani hapo na kushauri ni vema wote wanaohitaji ajira kufuata utaratibu.

Aliwataka wananchi hao kuwa wavumilivu kwani ndio kwanza kiwanda hicho kimeanza kazi na kitakuwa kinaajiri kwa awamu.

No comments