WABUNGE WAHOJI GHARAMA NYUMBA ZA NHC
Wakizungumza leo kwenye kamati za Bunge za Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wabunge hao wamehoji sababu zinazofanya nyumba hizo kuuzwa bei kubwa wakati lengo ni kusaidia wananchi.
Shirika la Nyumba Nchini (NHC) limekuwa gumzo mbele ya wabunge baada ya kuhoji kwanini nyumba zao zinakuwa za gharama ukilinganisha na taasisi nyingine
Wakizungumza leo kwenye kamati za Bunge za Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) wabunge hao wamehoji sababu zinazofanya nyumba hizo kuuzwa bei kubwa wakati lengo ni kusaidia wananchi.
Mbunge wa Tunduma (Chadema) Frank Mwakajoka amehoji ni kwasababu gani nyumba hizo zinauzwa bei kubwa.
"Ni sababu ya vifaa vinalipiwa kodi na nyumba nazo zinalipiwa kodi, mtuambie tubadilishe sheria ili tuondoe kodi ili nyumba ziweze kuuzwa kwa bei nafuu,"amesema
Yusuf Salim Hussein (Chambani-CUF) amesema kuwa katika eneo hilo wamepata miundombinu kama maji na umeme lakini bei ya nyumba bado ni kubwa ukilinganisha na zinazojengwa na taasisi ya Viguta.
"Kwanini bei ni kubwa hivyo. Lakini pia huku kujenga nguzo juu ni uchafu kwa ujenzi wa kisasa kwanini hamkupitisha umeme chini kwa chini?" amehoji.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Amina Mollel amesema kuna taasisi inayojulikana kama Viguta ambayo wanajenga nyumba zinazokaribiana na NHC lakini wanauza kwa bei ndogo ya kuanzia Sh 15 milioni.
"Utofauti ni gharama wao wanagharama ndogo na nyie ni kubwa wakati lengo lenu ni kuwasaidia Watanzania. Ni kwanini inakuwa hivyo?" amehoji.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Devotha Minja amesema japokuwa shirika hilo lina eneo kubwa katika mradi huo lakini hakuna nafasi ya kutosha kati ya nyumba na nyumba.
"Hapa mtasababisha ugomvi kuwa mwingi katika nyumba na nyumba kutokana na mwingiliano.kwanini hamkuweka space (nafasi) kati ya nyumba na nyumba wakati mna eneo la kutosha?"amesema.
Mbunge wa Kaliua(CUF) Magdalena Sakaya amesema kuwa kamati ilishatoa ushauri kuwa uwekezaji wa majengo ya shirika hilo uende kwa mtindo wa maghorofa lakini bado shirika hilo linajenga nyumba za chini.
"Kamati ilishatoa ushauri kuwa kutokana na idadi ya watu kuongezeka na ardhi haiongezeki mjenge maghorofa lakini bado mnajenga hivyo hivyo. Kwanini bado mnaendelea kujenga nyumba za chini?"amehoji.
Mbunge wa Mtama (CCM) Nape Nnauye alishauri shirika hilo kuongeza bidhaa zinazojali mahitaji ya mteja.
"Muangalie product (bidhaa) nyingine ambazo ni chaguo la mteja badala ya nyinyi kujenga na kuuza kama hivi zinaweza kutoka haraka,"amesema.
Amesema bidhaa hiyo inaweza kuwa kwa watu wenye viwanja lakini wakataka kujengewa na wao kulipa kidogo kidogo kwa ramani anayoichagua mteja mwenyewe.
Hata hivyo, wabunge hao walikubaliana kupokea majibu kutoka Serikalini kwa kuwa majibu hayo yalihitaji takwimu.
Awali Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Shirika hilo, Haikamen Mlekio amesema nyumba hizo zitauzwa kati ya Sh 68 milioni hadi Sh 99 milioni ukijumulisha na Kodi ya Ongezeko ya Thamani(VAT).
Amesema gharama ya mradi huo ambao umepanga kujengwa kwa nyumba 300 ni Sh 12.7 bilioni na kwamba hadu sasa wametumia Sh 6.9 bilioni kwa nyumba 151.
No comments