Breaking News

TUNDU LUSSU AFANYIWA OPERESHENI NYINGINE KWA MUDA WA MASAA SITA


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu jana alifanyiwa operesheni iliyochukua saa sita katika Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Hiyo ni operesheni takriban ya nne tangu aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi mchana wa Septemba 7 akiwa ndani ya gari nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma.

Jana, Rais huyo wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), aliingizwa chumba cha upasuaji kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tisa alasiri.

Mmoja wa madaktari walioshiriki katika operesheni hiyo, Dk Mushfiqur Khan alisema hali ya Lissu inaendelea vizuri.

Mbunge wa Tarime Vijiji, John Heche ambaye yupo jijini hapa alisema angeonana na Lissu jana jioni.

Maombi yaendelea

Wakati Lissu akiingia siku ya 18 ya matibabu hospitalini hapo, makanisa kadhaa nchini na Nairobi jana na juzi, yaliendelea na maombi kwa ajili yake.

Katika Kanisa la Wasabato la New Life, ambako Heche na katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche walisali, maombi yalifanyika.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza Heche alisema, “Tunashukuru wachungaji na viongozi wa dini hapa Kenya wamekuwa wakimuombea Lissu bila matatizo.”

Wakati maombi hayo yakiendelea huko Kenya, jana, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu aliwataka Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kumuombea Lissu kwa sauti hadharani na kwenye uzinduzi wa wimbo wa injili unaoitwa ‘Niliwahi simuliwa’ ambao umetungwa na kuimbwa na mwimbaji, Emmanuel Mwansasu katika Kanisa la Ebeneza Gospel lililopo Sokoine jijini Mbeya.

Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amesema kila Mtanzania kwa nafasi yake asimame na kumuombea Lissu kwa sauti, mahali pa siri, vilevile wamuombee hadharani kwa kuwa binadamu wote wanaunganishwa na ufalme wa Mola na si kitu kingine.

Nyalandu alitoa kauli hiyo jana mchana alipokuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa wimbo wa injili unaoitwa ‘Niliwahi Simuliwa’ ambao umetungwa na kuimbwa na Emmanuel Mwansasu katika sherehe zilizofanyika Kanisa la Ebeneza Gospel, Sokoine jijini Mbeya.

Uzinduzi huo uliambatana na maombi maalumu kwa ajili ya Lissu.

Alisema kilichotokea kwa Lissu kinaweza kutokea kwa mtu yeyote hivyo kinapaswa kulaaniwa na kila Mtanzania, huku akisisitiza kwamba jambo lolote linalotokea kwa mtu yeyote katika mazingira tatanishi linaigusa Taifa.

“Nimekuja Mbeya ili kufikisha ujumbe kwa Taifa kupitia kanisa hili kwamba katika kupigwa kwa mmoja wetu, tunakuwa tumepigwa sote, katika kuumizwa kwa mmoja wetu yeyote, tunakuwa tumeumizwa sisi sote, na katika kudhulumiwa kwa huyo mtu mmoja ni dhuluma dhidi ya Watanzania wote.

Kuhojiwa na CCM

Katika hatua nyingine, Nyalandu alikanusha taarifa zilizokuwa zimeenea kwenye mitandao ya kijamii zikidai kwamba ameitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya CCM kwa ajili ya kuhojiwa baada ya kwenda Nairobi kumjulia hali Lissu.

Alisema habari hizo ni za uongo na zimetengenezwa na watu wasiolitakia mema na kulifitinisha Taifa.

Wakati Nyalandu akisema hayo, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga alisema hana taarifa zozote za kuitwa kwa mbunge huyo kuhojiwa leo kwa sababu viongozi wake wametawanyika kwa shughuli za kikazi.

Lubinga alisema jambo hilo halipo kwa sababu yeye akiwa kiongozi hana taarifa hizo na haiwezekani Nyalandu akaitwa wakati hawapo ofisini.

“Hakuna mwenye habari hizo na kitu hicho hakipo. Sasa anaitwa wapi maana wote tumesambaa, mimi niko Morogoro, (Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey) Polepole yuko Arusha,” alihoji Lubinga.

Mbali ya kukanusha taarifa hizo, Nyalandu alisema, “Huu ni wakati wa Taifa kuwa pamoja watu kuungana. Huu ni wakati wa kuwa na mapenzi mema. “Hivi mimi natoka Singida Lissu kaka yangu anatoka Singida hivyo nishindwe kujitoa kwa sababu ya tofauti za siasa zetu? Hebu ifike mahala tuone mapenzi yetu ya Watanzania ni zaidi ya tofauti zetu za kiitikadi na vitu vingine lakini si ubinadamu na undugu wetu.”

Jana CCM ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Polepole ikisema vikao vya uongozi vya Taifa vinatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo inasema vikao hivyo vinavyofanyika kwa mujibu wa ratiba ya kawaida pamoja na mambo mengine, vitakuwa na kazi ya kujadili, kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho kwa wana CCM walioomba dhamana ya uongozi katika ngazi ya wilaya. Taarifa hiyo inasema Kamati Kuu itakaa Septemba 27 na 28 na Halmashauri Kuu ya Taifa itakaa Septemba 30 hadi Oktoba Mosi.

No comments