Breaking News

FISI AZUA BARAA HOSPITAL


Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Lucas David alisema fisi huyo alionekana saa kumi na mbili asubuhi bila kufahamu sehemu aliyopitia kuingia ndani na pia hakuna aliyejua alikotokea.

Wagonjwa na watumishi wa afya katika Hospitali ya Mji wa Kahama, juzi waliingiwa na taharuki na kutimua mbio ovyo baada ya fisi kuonekana asubuhi akirandaranda katika baadhi ya majengo ndani ya uzio wa hospitali hiyo.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Lucas David alisema fisi huyo alionekana saa kumi na mbili asubuhi bila kufahamu sehemu aliyopitia kuingia ndani na pia hakuna aliyejua alikotokea.

Alisema eneo la hospitali hiyo lina uzio mkubwa, lakini inawezekana fisi huyo alipitia eneo la chuo cha uuguzi ambako kuna matundu yaliyotobolewa na wanafunzi sehemu inayopakana na chumba cha maiti ambacho huenda lango la huko lilikuwa wazi.

Dk David alisema baada ya hali hiyo ya mtafaruku walitoa taarifa ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama na watendaji wa Idara ya Wanyamapori walifika hospitalini hapo na kumuua kwa risasi tatu hali ambayo ilituliza taharuki na kazi ndani ya hospitali hiyo ziliendelea kama kawaida.

Wilaya ya Kahama imekuwa na tatizo la kuzagaa kwa fisi ambao wanatishia maisha ya wananchi hasa wafugaji wanaolalamika mifugo yao kuliwa mara kwa mara na wanyama hao, huku jamii nyingine ikihusisha matukio ya kuzagaa kwa fisi hao na imani za kishirikina.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Juma Bakari alisema huenda mnyama huyo alisikia harufu inayotoka katika chumba cha kuhifadhia maiti.

“Huenda fisi huyo aliingilia huko kwa kufuata harufu kwa lengo la kula miili ya watu waliokufa na kuhifadhiwa huko, ndio maana alipitia maeneo hayo hayo,” alisema Bakari. Tukio la fisi huyo kuingia ndani ya hospitali limekuja baada ya Serikali mkoani Shinyanga kuanzisha msako wa kuwaua fisi katika halmashauri zote tatu za Wilaya ya Kahama kutokana na madhara yaliyosababishwa na wanyama hao kwa wananchi.


No comments