TFF YAINGILIA KATI KUAMUA MGOGORO WA YANGA KUHUSU TSHISHIMBI
Papy Kabamba Tshishimbi sasa anaweza kujimwaga kwa raha zake kuichezea Yanga baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumaliza utata uliojitokeza katika ishu yake ya usajili.
TFF imemaliza mgogoro wa kimasilahi kati ya wakala wa aliyekuwa kiungo wa Yanga, Justin Zullu ‘Mkata Umeme’, Karin Nir na uongozi wa Yanga, kufuatia kukatisha mkataba wa kiungo huyo.
Wakala huyo alipeleka mkataba wa mteja wake katika ofisi za shirikisho hilo akitaka kuizuia Yanga kumtumia Tshishimbi baada ya kukatishwa kiholela kwa mkataba wa Zullu.
Novemba, mwaka jana, Yanga ilimsainisha Zullu mkataba wa mwaka mmoja mbele ya wakala huyo raia wa Israel, lakini hivi karibuni Yanga iliachana naye kutokana na kiwango chake kutowaridhisha.
Nir amesema kuwa, TFF imetumia busara kulimaliza suala la mteja wake na Yanga kwani tayari alipanga kwenda kushitaki Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
“Nimeshaondoka Tanzania lakini jambo kubwa ni kwamba Yanga wamekubali kuvunja mkataba wa mchezaji wangu, mkataba umevunjwa kwa makubaliano ya pande zote mbili tena kwa usawa. Namshukuru Katibu Mkuu wa TFF kutokana na kuweza kulimaliza suala hili kwa amani, niwashukuru Yanga kwa kuonyesha ushirikiano hasa katibu wao, Boniface Mkwasa. Hatuwezi kuendelea na malumbano tena kati yetu kwani tutaendelea kushirikiana kama ilivyokuwa awali,” amesema Nir.
Justin Zullu alipanga kuishitaki Yanga Fifa ili alipwe dola 100,000 (Sh milioni 221) kwa kuvunjiwa mkataba wake kiholela.
No comments