TAMBWE: SIMBA BILA OKWI HAKUNA TIMU
Tambwe.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, amefurahishwa na matokeo ya bila kufungana ambayo Simba iliyapata juzi Jumamosi ilipocheza na Azam FC.
Hata hivyo, Tambwe ambaye msimu wa 2013/14 alikuwa akiitumikia Simba, alisema kuwa alijua kabisa timu hiyo isingepata matokeo mazuri katika mechi hiyo bila ya uwepo wa Mganda, Emmanuel Okwi kwenye mchezo huo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Tambwe alisema kuwa kwa washambuliaji wa Simba waliopo hivi sasa, ukimwondoa Okwi, ilikuwa ni ngumu kwao kuifunga Azam kutokana na kutokuwa na ubunifu wa kutafuta ushindi pindi wanapokuwa wamebanwa vilivyo na mabeki wa timu pinzani.
Emmanuel Okwi.
“Matokeo hayo nimeyapokea vizuri na nimefurahi baada ya kuona kile nilichokuwa nikiwaza akilini kwangu kimetimia, kwani nilijua kabisa Simba wangekutana na matokeo hayo katika mchezo huo.
“Hiyo ni kwa sababu washambuliaji wengi wa timu hiyo siyo wabunifu wa kutafuta mbinu mbadala za kufunga pindi wanapokuwa wamebanwa vilivyo na wapinzani wao.
“Mchezaji pekee ambaye angeibeba Simba katika mechi hiyo alikuwa ni Okwi lakini baada ya kusikia tu kuwa hatacheza mechi hiyo moja kwa moja matokeo hayo waliyopata yakanijia akilini kwangu,” alisema Tambwe na kuongeza:
“Kwa hivyo hivi sasa dalili ya sisi kuchukua ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya nne mfululizo nimeanza kuiona na ninamwomba Mungu nirejee mapema uwanjani ili niweze kuisaidia timu yangu ya Yanga kutimiza ndoto yetu hiyo.”
No comments