MSIGWA KULISHTAKI JESHI LA POLISI
Mbunge wa Iringa Mjini(Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema atalishitaki Jeshi la Polisi, kwa tuhuma za kuingilia majukumu yake ya kikazi pale anapokuwa akitimiza wajibu wake wa kibunge ikiwemo kuongea na wananchi.
Mchungaji Msigwa amesema atakata rufaa kwa sababu polisi wamezuia mikutano yake ya leo na kesho ambayo alitarajia kufanya katika kata za Kihesa na Kitwiru kwa madai ya kukiuka masharti alipohutubia katika Kata ya Mlandege.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Mchungaji Msigwa amesema chombo pekee kinachoweza kumtia hatiani kwa kufanya uchochezi ni Mahakama na sio polisi.
“Jana walinikamata tangu saa 11:30 na kuanza kunihoji mpaka saa 3:15 usiku kwa tuhuma za kufanya uchochezi lakini mimi nakataa sijafanya uchochezi kwa sababau hakuna mtu anaweza kunizuia kuongea na wananchi wangu, wanadai nimeleta hofu na kuvichonganisha vyombo vya dola na wananchi,” amesema Mchungaji Msigwa .
Amesema mpaka muda huu yupo nje kwa dhamana na tayari ameripoti polisi asubuhi leo Jumatatu amehojiwa lakini ameambiwa ataitwa tena kwa mahojiano zaidi.
“Mimi niko tayari hata kama wangeniweka ndani wiki mbili siogopi kwa sababu sitanyamaza nitaendelea kuongea na sitaacha kusema kilichomtokea Tundu Lissu na ili kuninyamazisha ni lazima waniue kwa sababu nishajiandaa kisaikolojia,” amesema Mchungaji Msingwa.
Akizungumzia hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi amesema walimkamata Msigwa kwa kuwa alikuwa anatoa maneno ya uchochezi kwa wananchi aliokuwa anawahutubia mkutano wa hadhara Kata ya Mlandege.
Mgengi amesema bado jeshi hilo linaendela na upelelezi juu ya tuhuma hizo na mara utakapokamilika watamfikisha mahakamani mbunge Msigwa.
No comments