Breaking News

MKUU WA WILAYA ASIMULIA JINSI ALIVYONUSURIKA KUCHARANGWA MAPANGA NA WANANCHI

HATIMAYE Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera Godfrey Mheluka, amesimulia namna alivyojinasua kutoka kwenye kundi la wananchi wenye hasira huku wakiwa na silaha za jadi ikiwamo mikuki, mishale na mapanga.

Vurugu hizo zilitokea wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipofika kijiji cha Kishanda, Kata ya Nyakahanga wilayani humo ili kutatua mgogoro wa ardhi ekari 132 iliyotekwa na mmoja wa wananchi.

Katika tukio hilo, diwani wa Kata ya Nyakahanga,  Charles Bechumila, alijeruhiwa vibaya kwa mkuki na hadi sasa hajaweza kujitambua tangu afikishwe hospitalini hapo.

DC huyo alisema walipofika tu eneo hilo, walijitokeza watu wengi wenye silaha na kuanza kuwashambulia, hali iliyosababisha kila mmoja aliyekuwa eneo hilo kukimbia ili kujinusuru.

"Mimi nilikuwa na walinzi wangu, askari watano na baadhi ya jeshi la akiba niliokuwa nimembatana nao… na ndio walionisaidia hata kumwokoa huyo diwani aliyejeruhiwa,"alisema Mheluka

Aliongeza kuwa walinzi aliokuwa nao walifyatua risasi juu, wananchi wakakimbilia vichakakani kujificha na ndipo walipopata fursa ya kumkimbiza diwani aliyejeruhiwa hospitali ili kupatiwa huduma.

Alisema kuwa awali, mkutano huo ulikuwa ufanyike kwenye kijiji cha Kishanda baada ya  ulioitishwa na diwani huyo. Muheluka alisema kuwa msafara huo uliongozwa na yeye, lengo likiwa ni kusikiliza kero zao na ghafla ndipo watu ambao hawakuonekana walipoanza kurusha mishale na mikuki kutokea vichakani.

“Tulikuwa tunaenda kuisikiliza kero. Kulikuwa na bwana mmoja anayejifanya kulimiliki eneo lenye ekari 132 na yeyote anayeingia pale anapigwa mapanga na mikuki,” alisema.

Watu kadhaa wameshakamatwa hadi sasa kuhusiana na tukio hilo, lakini kufikia mwishoni mwa wiki, mwandishi hakuwa na taarifa zaidi kuhusiana na operesheni hiyo

Katibu wa Hospitali Teule ya  Nyakahanga iliyopo wilaya ya Karagwe mkoani Kagera,  Jeremia Lugimbana, alisema diwani aliyejeruhiwa bado yuko kwenye hali mbaya.

Alisema baada ya kufikishwa hospitalini hapo, aliingizwa kwenye chumba cha upasuaji ili kuanza matibabu kwa  kumshona sehemu alizojeruhiwa

 "Alipoletwa hapa tulimpokea na kumuweka katika chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuanza kumtibu. Tulimshona majeraha akiwa hajitambui na hadi sasa hali yake bado ni hiyo," alisema Lugimbana

No comments